YANGA imekamilisha usajili wa mshambuliaji anayemudu pia kucheza winga zote, Jonathan Ikangalombo kutoka AS Vita, lakini taarifa ni kwamba nyota huyo mpya ametengenewa kucheza mechi za ndani tu za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) huku zile za kimataifa atakuwa mpenzi mtazamaji tu.
Ndio, Yanga imemsajili mchezaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili, lakini ni wazi hawezi kuitumikia timu hiyo katika mechi za kimataifa, hata kama Vijana wa Jangwani watavuka kwenye robo fainali wikiendi hii iwapo itaifunga MC Alger ya Algeria kwa vile alishaitumikia michuano hiyo akiwa na AS Vita.
Lakini wakati winga huyo akifunga usajili sambamba na beki wa kulia, Israel Mwenda, ingizo lake limemchomoa mshambuliaji Jeana Baleke kutokana na sheria inayotaka kila klabu kuwa na nyota wa kigeni wasiozidi 12 na Yanga tayari imeshakamilisha idadi hiyo kabla ya usajili huo mpya.
Winga huyo akiwa AS Vita alitumika katika michezo ya awali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini na kwa mujibu wa kanuni ya CAF mchezaji ambaye ametumika timu nyingine hawezi kuingizwa kwenye usajili hivyo atatumika kwenye ligi ya ndani pekee.
Ikangalombo alitumika katika mechi hizo za awali Kombe la Shirikisho ambapo AS Vita ilitolewa raundi ya pili na Wasauzi ambao wamepenya hadi robo fainali licha ya ushiriki wao wa kwanza katika michuano hiyo ya CAF.
Yanga Jumapili itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kuikabili MC Alger mchezo ambao umeshika hatma ya timu zote mbili kufuzu hatua inayofuata kutokana na kila moja kuwa na nafasi na winga huyo hatakuwa sehemu ya kikosi hadi msimu ujao kama timu yake itapata nafasi ya uwakilishi.
Kuhusu suala la Baleke ambalo Mwanaspoti ilishawahi kuripoti kuwa yupo kwenye mazungumzo na timu hiyo kuvunja mkataba wa kuendelea kubakia akiwa ameitumikia miezi sita huenda mwisho wake ukawa ndio huu kutokaba na idadi ya wachezaji kuongezeka.
Kabla ya kutambulishwa kwa winga huyo Yanga tayari ilikuwa na mastaa wa kigeni 12 kama kanuni inavyowahitaji ambao ni Djgui Diarra, Pacome Zouzoua, Prince Dube, Stephane Aziz Ki, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Attohoula Yao, Khalid Aucho, Chadrack Boka, Jean Baleke, Kenned Musonda na Clatous Chama.
Hivyo ni wazi kuwa kutambulishwa kwa Ikangalombo kunatoa mwanya wa Baleke kuondolewa kikosini kabisa kwani tayari aliacha kuonekana kwenye uwanja wa mazoezi lakini pia kwenye misafara ya timu hiyo ikiwa inaenda kupambania nembo ya klabu.
Baleke alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu tangu atue mchezaji huyo amekuwa akikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho akifanikiwa kufunga bao moja pekee.
Kuondoka kwa Baleke kunaifanya Yanga kutegemea nguvu ya washambuliaji watatu pekee ambao ni Dube anayeongoza kwa mabao akifunga mara nne, Mzize mwenye mabao matatu huku Kennedy Musonda aliye majeruhi akifunga mara mbili lakini pia ingizo jipya linaweza kuwa msaada kutokana na winga huyo kufiti kucheza na eneo la ushambuliaji.