ACT-Wazalendo yazindua timu ya ushindi 2025

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud amezindua timu ya ushindi ya chama hicho kwa upande wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Timu hiyo yenye wajumbe 15, inaongozwa na mwenyekiti Ismail Jussa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine, timu hiyo itaandaa mikakati ya kampeni na kusimamia ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2025.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 18, 2025 na Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma wa chama hicho, Salim Bimani, imesema mwenyekiti amewapongeza wateule wote kwa kuaminiwa kupewa jukumu hilo muhimu kwa mustakabali wa chama hicho na Taifa kwa ujumla.

“Kazi kubwa ya timu hiii ni kukipatia ushindi chama, kuinusuru Zanzibar na kuwapa fursa Wazanzibari kunufaika na ahadi ya ACT Brand Promise inayolenga kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika,” amesema.

Amesema katika uchagzui huo, hakuna mbadala zaidi ya ACT-Wazalendo kushinda na kwamba, hakuna namna ya kukubali hila za namna yoyote zitakazowanyima Wazanzibari chaguo lao.

Pamoja na Jussa, akisaidiwa na Yussuf Hamid ambaye ni makamu mwenyekiti, wajumbe wengine ni Omar Ali Saleh, Salim Bimani, Omar Said Shaaban, Nassor Ahmed Mazrui, Hafidh Abdulrahman Bakari, Mohammed Nur Mohammed, Muhene Said Rashid, Pavu Juma Abdallah,  Khamis Salim Ali, Janet Fusi, Fatma Abdulhabib Fereji, Nasra Said Nassor na Rashid Ali Abdallah.

Wajumbe hao watasaidiwa na wataalamu wa fani mbalimbali katika medani ya uchaguzi, teknolojia, uchumi, mawasiliano na wapigakura.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe hao, Jussa alimshukuru Othman kwa imani kubwa aliyowapa kuwa sehemu muhimu ya kuandika historia ya mabadiliko ya nchi.

Jussa ameahidi kuwa timu hiyo haitamuangusha na haitowaangusha Wazanzibari katika kutimiza matumaini yao na kuifikisha safari ya mabadiliko.

Related Posts