Dar es Salaam. Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) limemchagua Sharifa Suleiman kuwa mwenyekiti wake, matokeo yanayotajwa kuchora mstari wa mshindi wa nafasi ya uenyekiti Taifa wa chama hicho, Januari 21, 2025.
Katika uchaguzi ulioanza Januari 16 na matokeo kutangazwa usiku wa kuamkia leo Januari 18, uliokuwa na vitimbi na vurugu za mara kwa mara, Sharifa ameshinda kwa kura 222 dhidi ya 139 alizopata mshindani wake, Celestine Simba.
Ingawa matokeo hayo yanatajwa kuonyesha dalili za mshindi wa uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema taifa, kati ya Freeman Mbowe (mwenyekiti wa sasa) na Tundu Lissu (Makamu mwenyekiti -Bara), wataalamu wa sayansi ya siasa wanasema mambo bado hayatabiriki.
Bawacha ni baraza la mwisho la chama hicho kufanya uchaguzi, baada ya Baraza la Vijana (Bavicha) na la Wazee (Bazecha) kumaliza chaguzi zake Januari 14.
Vita ya uenyekiti wa Chadema taifa, itawakutanisha Mbowe, Lissu na Odero Charles katika uchaguzi utakaofanyika Januari 21, kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Matokeo yaliyompa ushindi Sharifa yalikuwa ya duru ya pili ya uchaguzi wa nafasi hiyo, baada ya kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote katika matokeo ya awali.
Katika matokeo ya awali, Sharifa alipata kura 167, Celestine kura 116 na Suzan Kiwanga kura 100.
Kabla ya nafasi hiyo, Sharifa alikuwa akikaimu wadhifa huo tangu mwaka 2020 baada ya aliyekuwa mwenyekiti, Halima Mdee na wenzake 18 kufukuzwa uanachama.
Matokeo ya uchaguzi huo, yalitangazwa saa 8:30 usiku wa kuamkia leo Januari 18 na mwenyekiti wa uchaguzi huo, Aida Kenani, ambaye pia ni mbunge wa Nkasi, mkoani Rukwa.
Alisema uchaguzi wa mwenyekiti wa Bawacha kura zilizopigwa ni 363 na kati ya hizo halali zilikuwa 361 na mbili ziliharibika.
Kenani alimtangaza Elizabeth Mwakimomo kuwa mshindi wa nafasi ya makamu mwenyekiti (Bara), aliyepata kura 212 sawa na asilimia 59, huku mpinzani wake Salma Kasanzu akipata kura 147.
Matokeo hayo ni ya uchaguzi wa marudio baada ya awali kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti -Zanzibar, Bahati Haji ameshinda kwa kura 212, dhidi ya 159 alizopata Zainab Bakari. Kura zilizopigwa zilikuwa 382, huku 12 ziliharibika.
Akizungumzia matokeo ya Bawacha na hatima ya uchaguzi wa Januari 21, mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Msonga amesema hayatakuwa na athari kubwa katika uchaguzi huo wa mwenyekiti wa taifa wa Chadema.
Amesema matokeo hayo si alama ya ushindi, badala yake mshindi atapatikana kwa kuzichanga karata zake vema kabla ya siku ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Msonga, washindi katika nafasi za kitaifa za mabaraza ni kura zinazojulikana uelekeo wake, lakini bado wao hawatoshi kuamua mshindi.
“Hawa washindi wa mabaraza wangekuwa na uwezo wa kuamua mshindi wa Januari 21, iwapo wangekuwa na muda wa kutosha wa kuwashawishi viongozi wa mikoa na majimbo wakamchague nani.
“Lakini kwa muda uliobaki kwa tathmini yangu sioni kama unatosha kwa viongozi hawa wapya kushawishi wapigakura kuchagua kambi wanazoziunga mkono,” amesema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema bado tathmini ya mshindi wa uchaguzi wa Januari 21, inabaki kuwa kizungumkuti.
Amesema mabaraza ya chama hicho yamegawanyika kila upande kati ya Lissu na Mbowe, ingawa Bazecha halitahiriki.
“Bado kutakuwa na ushindani na vigumu kutabiri matokeo. Kwa sasa matokeo ya chaguzi za mabaraza yanaweza kutoa matumaini kwa mgombea lakini kuna kazi kubwa. Bado sanduku la kura lina nguvu kwenye ushindi wa uchaguzi huo,” amesema.
Imechukua siku mbili kukamilisha mkutano mkuu wa uchaguzi wa Bawacha ulioanza Januari 16 hadi Januari 18, saa 9:15 usiku.
Uchaguzi wa Bawacha umekuwa wa mikesha miwili tofauti na wa Bavicha na Bazecha ambayo ilikuwa ya mkesha mmoja.
Mkutano wa uchaguzi wa Bavicha, ulianza Januari 13 na kutamatika jioni ya Januari 14, kama ilivyokuwa kwa Bazecha ulioanza siku moja na Bavicha na wenyewe ulimalizika asubuhi ya Januari 14.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa uchaguzi wa Bawacha, Kenani kura za marudio kwa baadhi ya wagombea na idadi kubwa ya walioomba ridhaa ya kuchaguliwa kwenye nafasi mbalimbali ni miongoni mwa sababu za hali hiyo.
Hata hivyo, Mwananchi ilishuhudia uchaguzi huo ukichelewa kuanza, hadi saa 5:00 usiku wa Januari 16, 2025 wajumbe hawakuwa wamehakikiwa.
Ingawa uchaguzi wa Bawacha uliwahusu wanawake, idadi kubwa ya waliokuwa nje ya ukumbi wa Ubungo Plaza ni vijana wa kiume.
Ukiachana na wale waliopewa nafasi ya kuimarisha ulinzi na itifaki katika maeneo hayo ya mkutano, walikuwepo wengine waliojitolea kulinda kisichojulikana.
Kutokana na mazingira hayo, ugomvi kati ya walinzi na vijana walioamua kwenda kukesha katika ukumbi huo, halikuwa jambo la kusubiri, mara kwa mara walijikuta wakirushiana makonde.
Kilichojificha nyuma ya yote hayo ni kile kinachodaiwa mapigano hayo yalikuwa kati ya wanaomuunga mkono Mbowe na wale wa Lissu.
Hata ugomvi baina yao, ulitokea katika nyakati za kila upande kusimamia ulinzi dhidi ya kambi nyingine isipate nafasi ya kucheza rafu ndani ya uchaguzi huo.
Ugomvi wa mara kwa mara ulisababisha Jeshi la Polisi lifike katika eneo hilo kuimarisha usalama, hata hivyo vijana wawili walitiwa nguvuni na gari moja lilikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Mburahati.
Hayo yalifanywa na vijana wa kiume nje ya ukumbi wa mkutano, ambao kimsingi si wahusika wa moja kwa moja wa uchaguzi huo.
Kwa wajumbe wa mkutano hali haikuwa shwari, haikupita nusu saa ya kila usiku wa uchaguzi huo, bila kushuhudiwa ama ugomvi wa ngumi au maneno katika korido za ukumbi huo.
Ugomvi wa mara kwa mara, ulichochewa na hali ya kutoaminiana kati ya kambi hizo mbili.
Katika mazingira hayo, madai ya rushwa halikuwa jambo la ajabu kusikika, kila wakati walituhumiana kwa rushwa hadi kupigana ngumi.
Kulikuwa na upande unaotaka uthibitisho wa kila lalamiko la rushwa, huku kambi nyingine ilisimama kuibua madai ya tendo hilo la jinai. Mvutano huo haukuwa mwepesi.
Dakika za mwisho kabla ya matokeo kutangazwa, tayari tetesi za ushindi wa Sharifa zilikuwepo.
Baada ya walinzi kuruhusu watu wote waingie ukumbini kusikiliza matokeo, ndani zilisikika nyimbo za ‘Mwamba, Mwamba, Mwamba’.
Makundi kwa makundi ya wajumbe yamfuata Sharifa kumkumbatia kumpongeza.
Yote hayo yalitangulia kisha matokeo yalitangazwa na shangwe la ushindi liliongezeka ukumbini, nyimbo zilizoimbwa na maneno yaliyosikika yalihusisha jina la Mbowe.
Akizungumza baada ya matokeo, Sharifa amewashukuru washindani wake, huku akieleza ushindi alioupata si wake bali wa chama hicho.
“Sitaweza peke yangu kuliongoza baraza hili ikiwa sitapata ushirikiano kutoka kwenu, naomba kushirikiana nanyi ili niweze kuliongoza baraza hili,” amesema.
Ameeleza hatua ya kwanza baada ya kushinda nafasi hiyo ni kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Sharifa amesema yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa yanapaswa kutazamwa kama funzo kwao na wajiandae vema na uchaguzi wa mwaka huu.
Kwa upande wa mshindani wake, Celestine amewashukuru wanawake 139 waliompigia kura ingawa hakushinda, kadhalika alitoa shukrani hizo kwa wengine wote waliopiga kura.
“Ukiwa kiongozi mzuri unaweza kuwakubali hata wale ambao wanaokupinga kwa hiyo ninawashukuru na najua wanajua kwamba nimepungua kidogo na mwenzangu amezidi kidogo,” amesema.
Hata hivyo, amesema ushindi huo ni wa Chadema na kwamba kilichosalia ni kuhakikisha wanaungana.
Kiwanga alipopewa nafasi hiyo amesema: “Hapo naona chama kimeshinda. Tuondoke hadi tarehe 21. Mimi bado Mjumbe wa Kamati Kuu, mtalisoma hilo Januari 21, tunakwenda kusimamisha chama.”