DILI la Rally Bwalya kutua Pamba Jiji limebuma baada ya viongozi wa Napsa Stars anayoichezea kumuwekea ugumu, huku mwenyewe akifunguka ameumia kushindwa kurejea kuja kucheza Ligi Kuu Bara.
Kiungo huyo Mzambia aliyewahi kuichezea Simba, msimu huu alitua Napsa iliyopo Ligi Kuu ya nchini humo na amecheza nusu msimu kabla ya Pamba Jiji kuanza kuihitaji saini yake dili ambalo hata hivyo limekufa.
Mwanaspoti liliwahi kuripoti usajili wa Bwalya bado haujaeleweka baada ya klabu ya Napsa kushindwa kutoa ushirikiano wa kulimaliza dili hilo hadi dirisha lilipofungwa juzi Jumatano.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Bwalya alisema ameumia kukwama kurudi Tanzania licha ya kutakiwa na Pamba lakini uongozi wa klabu anayoichezea uliweka ngumu kumwachia.
Alisema alishakubaliana kila kitu na Pamba lakini ishu ikabaki kwa klabu na wakashindwa kuafikiana juu ya ada ya uhamisho.
“Bado nina kiu ya kurejea Tanzania kwa kuwa ni sehemu ambayo naamini ushindani ni mkubwa na kunaweza kumfanya mchezaji yeyote atakayejielewa kucheza soka la mafanikio litakalomkuza. Nimeumia sana kushindwa kuja huko ila kama riziki bado ipo nikimaliza mkataba basi, nitapata timu na kurejea kwa mipango ya Mungu.”
Pamba iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, inashika nafasi ya 14 katika msimamo na imesajili wachezaji kutoka nje ambao hata hivyo bado hawajawatanga licha ya dirisha dogo kufungwa Januari 15.