Kauli ya Polisi kifo cha mwanahabari

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema Charles Mwita, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari aliuawa kwa kushambuliwa na watu ambao walitokomea baada ya kutenda tukio hilo katika eneo la Nyamisangora, Kaunti ya Migori nchini Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana Januari 17, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, tukio hilo linashughulikiwa nchini Kenya kulingana na sheria za Taifa hilo.

Awali, taarifa kutoka familia ya Mwita (48), ilisema ndugu yao amefariki dunia ikidaiwa amepigwa risasi na watu wasiojulikana saa moja usiku wa Julai 16, eneo la Kata ya Sirari wilayani Tarime, mkoani Mara.

“Jeshi la Polisi limefuatilia kwa karibu sana taarifa hii na kubaini hakuna tukio la namna hiyo ambalo limeripotiwa kutokea maeneo ya Tarime na hata maeneo mengine mkoani Mara.

“Jeshi la Polisi katika ufuatiaji zaidi na kwa kutumia mahusiano mazuri ya ujirani mwema kati ya Polisi Kenya na Tanzania zipo taarifa kuwa kuna mtu ambaye amefahamika kwa jina la Charles Chacha Mwita aliuawa kwa kushambuliwa na watu ambao walitokomea baada ya kutenda tukio hilo katika eneo la Nyamisangora, Kaunti ya Migori, Kenya na wanalishughulikia kulingana na sheria zao,” imesema taarifa ya polisi.

Mwita, ambaye alikuwa mbobezi wa habari za uchumi na biashara amewahi kuzitumikia kampuni tofauti za habari nchini ikiwemo The Guardian Limited na Mwananchi Communications Limited (MCL). Amefanya kazi MCL kwa takribani miaka saba.

Mdogo wa marehemu, Nelson Mwita akizungumza na Mwananchi jana Januari 17, 2024 alisema:

“Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wanadai kaka alivamiwa na watu watatu wasiojulikana kisha wakampiga risasi kadhaa na kutokomea kusikojulikana, hata hivyo tayari tukio hilo tumesharipoti polisi kwa ajili ya hatua zingine.”

“Ni tukio ambalo limetokea ghafla bado familia hadi sasa haijakaa kupanga taratibu za mazishi,” alisema.

Alipotafutwa Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, Mark Njera kuzungumzia tukio hilo  alisema hakuna taarifa ya tukio hilo lililoripotiwa katika vituo vya polisi eneo hilo.

Mwita alijiunga na Mwananchi mwaka 2010 kama Mhariri Msanifu, alihudumu kwa miaka saba katika vipindi viwili vilivyomalizika mwaka 2019.

Related Posts