Konokono wazua balaa mashambani Mbeya

Mbeya. Wakulima Mikoa ya Songwe na Mbeya wamejikuta katika taharuki kufuatia konokono kushambulia na kuharibu mazao yao shambani.

Changamoto ya viumbe hao inatajwa kuanza kutokea tangu mwaka jana ambapo athari haikuwa kubwa kulinganisha na mwaka huu ambapo mvua zinaendelea kunyesha.

Wakizungumza na Mwananchi leo Januari 18, baadhi ya wananchi waliokumbwa na uharibifu huo wamesema bado hawajajua kiini na chanzo kikubwa cha wadudu hao, huku wakianza kuchukua tahadhari zilizotolewa na wataalamu.

Sikujua Msukwa mkulima na mkazi wa Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe amesema kwa sasa hali imekuwa mbaya shambani kwa wadudu hao kuharibu mazao haswa mibuni.

Amesema wadudu hao walianza kuonekana tangu mwaka jana lakini hawakuwa katika wingi huo, ila kwa sasa wanaokota ndoo nne hadi sita kwa siku hali inayotishia shughuli za kilimo.

“Tuliripoti changamoto hii tunashukuru wataalamu wamefika kutoka wizarani, wametupa maelekezo namna ya kukabiliana nao na tiba ya kiuatilifu tunachotumia kuona kama kitasaidia” amesema Msukwa.

Muonekano wa mkahawa ulioshambuliwa na wadudu aina ya konokono.

Naye Omary Mlungu mkazi wa Isenzanya wilayani Mbozi mkoani humo, amesema uharibifu wa viumbe hao ulianza misimu mitatu nyuma, japokuwa umeshika kasi mwaka huu baada ya mvua iliyonyesha.

Amesema kwa sasa wanaendelea kutumia viuatilifu walivyopewa na wataalamu kutoka mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA) ili kuona matokeo.

“Hii dawa tuliyopewa inachukua siku tatu kuona matokeo yake, kwa ujumla ni changamoto katika mazao haswa kahawa kwa kuwa wanabangua na kuacha mti” amesema Mlungu.

Kwa upande wake Deus Mwayela mkazi wa Mbeya Vijijini, amesema wadudu hao wamekuwa tishio katika mazao akieleza kuwa bado hawajapata sababu za mlipuko wa wadudu hao.

“Kwa kuwa Serikali imefika kuona na kutoa maelekezo tunaanza matumizi ya kiuatilifu kina aina ya fangasi hivyo tunasubiri kuona baada ya siku tatu hali itakuwaje” amesema Mwayela.

Wataalamu wa kilimo wakiwamo maofisa kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA), wakitoa maelekezo kwa baadhi ya wakulima mkoani Songwe waliokumbwa na janga la wadudu hao.

Ofisa Ugani Wilaya Rungwe, Boniface Mwambele amesema matarajio yao ni kuona wanatokomeza wadudu hao baada ya kubaini kiuatilifu aina ya Bio side na kwamba sababu kubwa ni mabadiliko ya tabianchi.

“Hii aina ya dawa kutoka Plant Bio Defender, ina nguvu na kazi yake ni kukausha wadudu hao, matarajio yetu ni kuona mkulima akiendelea na kilimo chake” amesema Mwambele.

Mkuu kitengo cha milipuko ya visumbufu ya mazao kutoka TPHPA, Grace Matiku amekiri kuwapo changamoto hiyo na kwamba walipata kilio cha wakulima tangu mwaka jana.

Amesema pamoja na kuripotiwa ugonjwa huo, lakini mamlaka haikuwa na kiuatilifu chochote badala yake wamefanikiwa kupata aina ya Bio side na wamesambaza kwa wakulima na kuomba watakaokumbana na changamoto kuwasiliana na mamlaka hiyo.

“Kilio kilitokea kwa wakulima kutoka mikoa minne nchini ikiwa ni Mbeya, Songwe, Pwani na Arusha na tayari tumefika kwa wakulima wenyewe baadhi na kuona hali ilivyo na tunaendelea kuwafikia waathirika wote”

Grace ameongeza kuwa, “kwa maeneo tuliyotoka Mbozi na Mbeya Vijijini ni wakulima  21 na bado tunatarajia kufika Rungwe, kisha Pwani na kumalizia Arusha, niwaombe wenye tatizo hili wasisite kuwasiliana na TPHPA.”

Related Posts