Maswa yapitisha bajeti Sh47.2 bilioni

Maswa. Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, limepitisha Sh47.2 bilioni kama rasimu ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Hayo yamebainika leo Jumamosi Januari 18, 2025katika kikao hicho cha bajeti kilichofanyika Maswa.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Simon Maige ametoa wito kwa madiwani kusimamia vizuri miradi inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo ikiwamo ya afya, elimu, kilimo, mifugo na maendeleo ya jamii.

“Ili tutekeleza vizuri bajeti ijayo, tunahitaji kukamilisha miradi yote ambayo tumeipanga hasa kupitia mapato ya ndani,” amesema Maige huku akisisitiza kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Amesema katika kutekeleza miradi ya kimkakati, inatakiwa ushirikiano na usimamizi mkubwa wa makusanyo ya mapato na kupeleka fedha kwa wakati katika miradi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Maisha Mtipa amesema halmashauri hiyo imekamilisha mradi wa kimkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha chaki kinachotarajiwa kuingiza gawio la Sh147.7 milioni kwa mwaka.

Amesema katika kuhakikisha wanakusanya mapato, pia wameunda kikosi kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato kwa kuajiri vijana 10 kwa mikataba watakaokusanya mapato maeneo ya minada, magulio na vituo vya kuuzia mazao ya kilimo.

Diwani wa Nyalikungu, Joseph Bundala ametaka usimamizi mzuri wa kiwanda cha kutengeneza chaki katika uzalishaji sambamba na utoaji wa ajira kwa vijana.

Mohamed Dasse ambaye ni diwani wa Sengwa, amesema ni vizuri kubuni vyanzo vipya vya mapato vikiwamo kwenye michezo hasa mpira wa miguu  na mabonanza yanayokusanya fedha.

“Tubuni vyanzo vipya vya kuivusha Wilaya ya Maswa ili kufikia matokeo makubwa, kwa sasa mchezo wa mpira wa miguu unachezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu na wanakusanya, tusidharau hiki ni chanzo cha mapato,” amesema.

Related Posts