Mserbia apewa masharti KenGold | Mwanaspoti

KenGold imefikia makubaliano ya kumpa mkataba wa miezi sita kocha mpya raia wa Serbia, Vladislav Heric iliyomtambulisha jana Jumamosi, huku akipewa masharti ya kuhakikisha kikosi hicho chenye makazi yake Chunya jijini Mbeya, kinasalia Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Kocha huyo wa zamani wa Chippa United ya Afrika Kusini, aliwasili nchini juzi kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho, huku akikutana na viongozi na wachezaji na kuwaomba ushirikiano ili kwa pamoja wafikie malengo waliyojiwekea kwa msimu huu.

Mmoja wa nyota wa timu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake kutokana na kocha huyo kutotangazwa na klabu, aliliambia Mwanaspoti, Heric ametakiwa kukipigania kikosi hicho huku akiwaahidi wachezaji wote kuwapa ushirikiano bila ya kujali.

“Amesema hatojali ukubwa wa jina la mchezaji yeyote kikosini zaidi ya kututaka wote kuheshimiana na kucheza kwa kujitoa kwa ajili ya klabu, pia amesisitiza nidhamu ndiyo kipaumbele chake kikosini,” alisema mmoja wa wachezaji wa kikosi hicho.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa KenGold, Benson Mkocha alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia ujio wa kocha huyo, alisema kama kukiwa na maboresho yoyote yanayohusu klabu hiyo wataweka wazi, ila kwa sasa tusubiri kuona kitakachojiri.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa timu hiyo aliliambia Mwanaspoti, Heric licha ya kupewa kwanza mkataba wa miezi sita ila ataongezewa mwaka mmoja zaidi, ikiwa tu KenGold inayoburuza mkiani na pointi zake sita itasalia Ligi Kuu kwa msimu ujao.

Mbali na kuifundisha Chippa United, timu nyingine ni Club Africain ya Tunisia, Maritzburg United, Ubuntu Cape Town, Bay United, Polokwane City, FC Cape Town, Black Leopards, African Warriors na Cape Town Spurs zote kutokea Afrika ya Kusini.

Kocha huyo aliyezaliwa Agosti 29, 1966, ameifundisha pia Royal Eagles ya Afrika Kusini, akianza kucheza mwaka 1976 akiwa na akademia ya FK Vojvodina’s, huku soka la kulipwa akizichezea timu za FK Proleter Novi Sad na FK Fruskogorac Novi Sad.

Heric ambaye ni mzoefu wa soka akiwa na Shahada katika Chuo Kikuu cha Novi Sad cha kwao Serbia, ana leseni ‘A’ ya UEFA na aliacha kucheza soka la ushindani akiwa na miaka 21 tu, baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Related Posts