Pamela Maasay katibu mpya Bawacha

Dar es Salaam. Pamela Maasay amechaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) akimbwaga Catherine Ruge aliyeshindwa kutetea nafasi hiyo.

Katika kinyanganyiro hicho Catherine alipata kura 34 sawa na asilimia 40, mgombea mwingine Esther Daffi akipata kura 15, Pamela akiibuka kidedea mbele ya washindani hao wawili kwa kura 37 sawa na asilimia 54.

Uchaguzi uliompa ushindi Maasay kuwa katibu wa Bawacha umefanyika leo Januari 18, 2025 Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Mbali na nafasi hiyo, Nuru Ndosi ametetea nafasi yake na naibu katibu Taifa-bara  kwa kura 42 akimuangusha mpinzani wake wa karibu Glory Latamani aliyepata  kura 31 na Neema Mhanuzi akipata kura 11.

Upande wa uwakilishi wa nafasi ya naibu katibu Taifa –Zanzibar,  Asiata Abouubakar alitangazwa kushika nafasi hiyo kwa kura 65 huku akipigiwa kura 19 za hapana.

Kwa upande wa nafasi ya mratibu uenezi Taifa, Aisha Machano ameshindwa kutetea nafasi hiyo akipata kura 41 akiangushwa na Sigrada Mlingo aliyepata kura 42.

Katika matokeo yaliyotangazwa usiku wa kuamkia leo Januari 18, 2025 Sharifa Suleiman ametangazwa kuwa mwenyekiti wa Bawacha akipata kura 222 dhidi ya kura 139 alizopata mshindani wake, Celestine Simba.

Matokeo ya ushindi wa Sharifa yalikuwa ya awamu ya pili ya uchaguzi wa nafasi hiyo, baada ya kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, katika matokeo ya awali.

Katika matokeo ya awali, nafasi hiyo iliyokuwa inagombewa na Sharifa akipata kura 167, Celestine kura 116 na Suzan Kiwanga akiambulia kura 100.

Kabla ya nafasi hiyo, Sharifa alikuwa akikaimu wadhifa huo tangu mwaka 2020 baada ya aliyekuwa na nafasi hiyo, Halima Mdee na wenzake 18 kufukuzwa uanachama.

Matokeo ya uchaguzi huo, yalitangazwa jana na mwenyekiti wa uchaguzi huo, Aida Kenani ambaye pia ni mbunge wa Nkasi, Rukwa.

Kenani alisema uchaguzi wa mwenyekiti wa Bawacha ulikuwa na jumla ya wapigakura 363, kati ya hizo halali zilikuwa 361 na mbili ziliharibika.

“Kwa mamlaka niliyopewa namtangaza Sharifa Suleiman kuwa mwenyekiti wa Bawacha Taifa,” alisema na kuibua shangwe kutoka kwa wana-Chadema waliokuwepo ukumbini hapo.

Matokeo mengine yaliyotangazwa ni makamu mwenyekiti bara na Zanzibar na wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu Bawacha.

Kenani alimtangaza Elizabeth Mwakimomo kuwa mshindi wa nafasi ya umakamu uenyekiti bara akipata kura 212 sawa na asilimia 59, huku mpinzani wake Salma Kasanzu akipata kura 147.

Kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar, Bahati Haji ameshinda kwa kura 212, dhidi ya 159 alizopata Zainab Bakari.

Wapigakura wa nafasi hiyo walikuwa 382, huku kura 12 zikiharibika.

Mweka hazina Bawacha nafasi hiyo amechaguliwa Joyce Mukya kwa kura 49 na Brenda Jonas akipata kura 35.

Related Posts