Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ameeleza kukerwa na tetesi za mitandao ya jamii ilivyovumisha jina lake kuwa miongoni mwa wanaotajwa kuwa makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara.
Nafasi hiyo imeachwa wazi na Abdulrahman Kinana aliyeomba kustaafu Septemba 2024.
Tayari chama hicho kimeshamtaja kada mkongwe Stephen Wasira kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza leo Januari 18, 2025 katika Mkutano Mkuu wa CCM jijini Dodoma, Pinda amesema hivi karibuni kumekuwa na tetesi ya jina lake kutajwa kuwa miongoni mwa watakaorithi nafasi hiyo.
“Sina budi kusema kwa sababu ya mitandao hii eeh! Wakati mwingine inakutoa jasho. Unafikiri labda kuna mmoja kanong’onezwa kwamba wewe mzee ndio unakwenda kuwa makamu, kumbe wapi, kumbe sivyo,” amesema.
Pinda aliyeongoza ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) kuangalia uchaguzi wa Botswana mwishoni mwa mwaka jana, amesema aliitwa na Rais Samia Suluhu Hassan na wajumbe wenzake.
“Mimi ndio niliitwa wa kwanza nikaingia hapo, nikamsimulia mambo yalivyokwenda vizuri, mwishoni nikawa nimemaliza nikabaki namsikiliza ili aseme kama hii mitandao inavyoeneza, lakini hakufanyika hivyo.
“Lakini kumbe ndivyo ilivyo, sasa unataka akwambie siri halafu utoke uanze kuropoka? Hapana, kwa hiyo nimetoka mle, not so happy (siko na furaha hivyo), lakini nikasema angalau amenipa meseji,” amesema.
Amesema baada ya kutoka kwa Rais Samia akarudi kuangalia mitandao, akakuta minong’ono zaidi.
“Ukirudi mitandaoni, mama yangu mama yangu, waliona sijui nimepiga picha na nani, wakasema aah kumbe alikuwa ameitwa huko, nikawaambia aah, mngejua!”
Hata hivyo, baada ya kutajwa Wasira, Pinda amesema ameshukuru kwa kuwa mambo yameisha.
Akimzungumzia Wasira, Pinda amesema wamekuwa wakifungana katika minong’ono ya uteuzi, akirejea mwaka 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Edward Lowassa kujiuzulu.
“Wala si kwamba unaambiwa omba fomu, hapana, mitandao tu ikaibuka na zake, Mizengo Pinda, Wasira, nani nani eh! Kila ukikutana na mzee mmoja atakumegea siri, hakuna hata mmoja, kwa hiyo na sasa limekuja limetokea leo,” amesema.
Pinda aliyefanya kazi na Wasira, amemwelezea kama mchapa kazi na mwenye historia ya muda mrefu ya siasa tangu Tanu mpaka CCM.
“Mimi sina shaka na uwezo wa huyu mzee hata kidogo, kwa sababu nimekuwa naye karibu ndani ya chama, hata tulipokuwa serikalini bado tumefanya kazi pamoja,” amesema.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuachana na upambe wa magazeti na mitandao, bali waungane kumsaidia mwenyekiti na makamu wa CCM.
Awali, akitoa azimio liliopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM, Naibu katibu mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Dk Mohamed Said Dimwa amesema tabia, mwenendo na sifa za Wasira ndizo zilizosababisha halmashauri kuu ya chama hicho, kumteua awanie umakamu uenyekiti wa CCM (bara).
“Halmashauri Kuu ya CCM, imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha pasipo shaka kuhusu tabia, mwenendo, tabia na sifa za mwanachama huyo kwa muda wote wa uhai ndani ya CCM.
“Pia, anazingatia kikamilifu masharti ya wanachama, sifa na miiko ya kiongozi kama ilivyoanishwa katika ibara ya 8, 17 na 18 za katiba ya CCM, daima amekuwa mstari wa mbele kupigania, kulinda masilahi ya chama chetu, umoja na mshikamano wa kitaifa.
“Ni mkweli, mnyenyekevu, anayependa nchi yake ni mtiifu ndani ya CCM na raia mwema,” amesema.