Sababu tatu za ushindi Yanga

Yanga kwa namna yoyote ile inatakiwa kupata ushindi katika mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 10:00 jioni.

Sababu tatu zinailazimisha Yanga kupata ushindi leo ambazo ni kufuzu robo fainali ya mashindano hayo, kulipa kisasi na kumaliza unyonge ilionao dhidi ya MC Alger na mwisho ni kusogea hadi nafasi ya tano katika chati ya ubora wa klabu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), kutokana na pointi ambazo timu huvuna katika kipindi cha miaka mitano ya ushiriki kwenye mashindano ya klabu Afrika.

Ushindi katika mchezo huo utaifanya Yanga ifikishe pointi 10 na hivyo kuungana na Al Hilal kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo kutokea Kundi A.

Kinyume na hapo, Yanga itakomea katika makundi na MC Alger kusonga mbele ikiwa mechi ya leo itaisha kwa matokeo ya sare au kama wawakilishi hao wa Tanzania watapoteza mechi hiyo.

Ikiwa itafanya hivyo, maana yake Yanga itajihakikishia kuvuna kitita cha Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni) ambazo kila timu inayofikia hatua hiyo inakuwa na uhakika wa kupata kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Hata hivyo, ifahamike kwamba Yanga ikipata ushindi leo haitoweza kuongoza kundi A, hata kama Al Hilal itapoteza dhidi ya TP Mazembe kwa vile Yanga itaangushwa na kigezo cha kutofanya vizuri katika mechi mbili dhidi ya Al Hilal.

Sababu ya pili ni kufuta uteja ambao Yanga imekuwa nayo dhidi ya MC Alger ambapo imekuwa haina historia nzuri dhidi ya timu hiyo ya Algeria.

Katika mara tatu za nyuma ambazo timu hizo zimewahi kukutana siku za nyuma, MC Alger imepata ushindi mara mbili huku Yanga ikishinda mechi moja.

Lakini pia ni fursa nzuri kwa Yanga kurudisha kichapo ambacho ilikipata katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo jijini Algiers, Algeria ambao ulimalizika kwa wenyeji MC Alger kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Yanga pia itaishusha Simba na kusogea hadi nafasi ya sita katika chati ya ubora wa klabu Afrika kwa muda wa miaka mitano ya Caf kwa vile Simba itakuwa na pointi 38.

Ikitinga robo fainali, Yanga itapata pointi tano ambazo zitazidishwa kwa tano kupata 15 na kisha kujumlishwa na pointi 24 ambazo Yanga imezivuna katika misimu minne iliyopita kutegemeana na mafanikio iliyoyapata katika mashindano ya kimataifa kufanya iwe na pointi 39, ambazo ni sawa na za Wydad ambayo itakuwa katika nafasi ya tatu.

Tegemeo kubwa kwa Yanga katika mechi ya leo ni kiungo wake Stephane Aziz Ki ambaye ndio anaongoza kwenye kikosi chao kwa kuhusika na mabao mengi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa amefanya hivyo mara mbili lakini pia ndiye mchezaji anayeongoza kwa kupiga mashuti kwenye hatua hiyo ambapo kwa kila mchezo ana wastani wa kupiga mashuti 5.6 kwa mchezo.

Soufiane Bayazid ndio mchezaji hatari zaidi katika kikosi cha MC Alger kwani naye amehusika na mabao mawili kama Aziz Ki. Refa kutoka Mauritania, Patrice Milazar ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo ya leo.

Mchezo mwingine wa kundi hilo leo utakuwa huko Lubumbashi, DR Congo ambako TP Mazembe ambayo haina matumaini itaikaribisha Al Hilal ambayo imeshafuzu ikiwa kinara wa kundi.

Related Posts