Dar/Mikoani. Ukomavu katika siasa, misimamo katika ukweli, ushupavu wa uongozi na uchapakazi vinatajwa kuwa sababu ya Stephen Wasira kuteuliwa na kisha kuchaguliwa kuwa makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara.
Wasira ametangazwa kushika wadhifa huo na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan baada ya uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete leo Januari 18, 2025 jijini Dodoma.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kura zilizopigwa katika uchaguzi huo ni 1,921, huku kura nne zikiharibika.
Amesema kura halali kwenye uchaguzi huo zilikuwa 1,917 na Wasira alipata kura 1,910 sawa na asilimia 99.42 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi huo huku saba zikimkataa.
Wasira, mwanasiasa mkongwe aliyehudumu katika awamu zote za Serikali nchini, anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana aliyejiuzulu wadhifa huo.
Uteuzi wake ni kielelezo cha kuendelea kung’aa kwa nyota yake kwenye uongozi, sambamba na kusadifu kauli ya ‘Bado yupo’ iliyowahi kutolewa Makongoro Nyerere ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Makongoro alitoa kauli hiyo wakati wa mchakato wa kura za maoni za CCM alipokuwa akiwania kuteuliwa kuwa mgombea urais mwaka 2015, akisimulia jinsi Wasira alivyoanza kufanya kazi tangu awamu ya kwanza ya Serikali ya Tanzania.
Mjumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM uliomchagua Wasira, Luhaga Mpina amesema chama hicho kimepata kiongozi sahihi kwa kuwa ana uzoefu wa kutosha na kwa tabia yake ya kusema ukweli wakati wote.
“Tunaamini atasimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kudhibiti wala rushwa na wabadhirifu wa mali za umma,” amesema Mpina ambaye pia ni mbunge wa Kisesa.
Mjumbe mwingine wa mkutano huo, kutoka Arumeru Magharibi, Ezeckiel Mollel amesema Wasira ni mtu muhimu, amejaa hekima, mahiri na hata wapinzani wanafahamu umahiri wake katika uongozi.
“Hiki ni kielelezo kuwa ndani ya CCM kumejaa hazina ya viongozi wengi. Kupitishwa kwa Wasira ni kidhihirisho tosha kuwa katika uchaguzi ujao tunaenda kushinda kwa kishindo,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Louisuile amesema kiongozi huyo amekuja katika wakati wake mwafaka.
“Naona CCM wamepatia, kwa sababu kiongozi anayetakiwa katika nafasi hiyo siyo mtendaji wa kila siku, bali ni mtu anayemsaidia mwenyekiti kutekeleza majukumu yake,” amesema.
Amesema nafasi hiyo haikuhitaji mtu mwenye ndoto ya kuja kuwa na nafasi nyingine ya kisiasa, kwa hiyo ni sahihi kwa Wasira.
Mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza amesema kwa kuwa ni chama kilichoshika madaraka, Wasira hawezi kuleta mchango mkubwa kwa Watanzania.
Amesema licha ya Wasira kuwa mtumishi wa umma na katika nafasi za siasa kwa muda mrefu, bado hajaonyesha mchango mkubwa kwa Taifa hasa katika sekta ya uzalishaji inayotegemewa na Watanzania wengi.
Naye Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, amesema Wasira ni kama baba na mlezi aliyelea vijana wengi wa CCM na kuwapa ushauri.
‘’Kwa uteuzi huu, chama kimelamba dume. Wasira ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kukisemea chama hicho katika majukwaa na kujenga hoja,’’ amesema.
Mjumbe mwingine wa mkutano huo, Nape Nnauye amesema CCM imepata makamu mwenyekiti mwenye uzoefu wa kujenga hoja, akisema Wasira ni bingwa wa suala hilo.
“Wasira ni mtu mkweli ambaye kukwambia umevaa vibaya haoni shida, ninaamini tumepata mtu atakayekipeleka chama mbele na kutuvusha salama katika uchaguzi,” amesema Nape ambaye ni mbunge wa Mtama.
Wasira amewashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumchagua, akisema anaianza kazi kwa kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushinda katika uchaguzi na kushika dola.Pia, amesema atahakikisha anasimamia umoja, amani na maendeleo.
“Kazi ya chama hiki imeelezwa kwenye ibara ya 5 ya Katiba ya CCM, ambayo ni kushinda uchaguzi kukamata dola ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar na serikali za mitaa,” amesema.
Amesema kwa sasa wameshashinda uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, lakini bado kazi iko mbele.
“Sasa kazi tuliyonayo ni kukamata dola ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar. Ndugu zangu, Waislamu wanasema kanzu ya Ijumaa inafuliwa Alhamisi, sasa hivi wamebadilisha wanasema tufue Jumatano, sasa Jumatano imeshapita tumechukua serikali za mitaa. Sasa tujiandae ikifika Oktoba kazi ya kuchukua dola ikamilike,” amesema.
Amesema ili kushinda watajinadi kwa kueleza utekelezaji wa ahadi walizotoa.
“Tumejenga shule kila mahali, tunatua ndoo kina mama kichwani kila mahali, halafu miradi ya maendeleo tuliyoambiwa baada ya Rais John Magufuli kututoka akakabidhiwa Samia, sasa reli ni mpaka Dodoma..
“Kuna daraja linaitwa la Magufuli kule Busisi (Mwanza) linakamilika, kuna bwawa la umeme linakamilika, kama hivyo ndivyo twendeni tukashinde basi, maana sababu za kushinda zipo, nia ipo na uwezo tunao,” amesema.
Kazi ya pili atakayoitekeleza amesema ni kutangaza kwa dunia na Watanzania wajue kwamba CCM ni chama cha amani na maendeleo.
“Ndiyo ajenda zetu, tunapewa nchi ili tufanye maendeleo, lakini huwezi kufanya maendeleo bila amani, maana amani ndiyo msingi wa maendeleo,” amesema.
Kuhusu maridhiano, amesema ataendeleza maridhiano ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R inayomaanisha maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), Ustahilimivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding), ambayo imeanzishwa na Rais Samia.
“Wengine wanasema maridhiano hakuna ile ni falsafa haturidhiani na mtu mmoja, tunaridhiana na jamii. Na jamii ina wadau wengi ina viongozi wa kiroho wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii za kimataifa wanaoishi hapa,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Kinana amesema hana shaka katika uchaguzi mkuu ujao chama hicho, kitampendekeza Rais Samia awanie nafasi hiyo. Amewataka wana-CCM kumuunga mkono Samia.
Amesema makada wa chama hicho wanampenda mwenyekiti wao na kuthamini kazi kubwa anayofanya ya kujituma na kujitolea kutekeleza ilani ya chama hicho na kutimiza ahadi anazotoa kwenye ziara.
“Sina shaka hata kidogo katika uchaguzi mkuu ujao, wana-CCM watampendekeza na Watanzania watamchagua ili kupata maendeleo makubwa zaidi,” amesema.
Kinana aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, amewashukuru pia wajumbe wa kamati kuu ambao kwa muda wote waliopitisha jina lake, akisema kama kuna sifa alizozipata katika utumishi wake ndani ya chama basi ziende kwa wana-CCM kwa sababu chama hicho siyo cha viongozi bali cha wanachama.
“Ndugu mwenyekiti uliponiandikia barua kunitaka niwe tayari kuendelea kushirikiana na wana-CCM wenzangu katika kufanya kazi, nilikuahidi mbele yako na mkutano mkuu kuwa nitatimiza ahadi hiyo,” amesema.
Kuhusu Wasira, amesema ni mtu hodari na mchapakazi, mwadilifu na mzalendo kwa Taifa, akisema ana uhakika nafasi ya umakamu ipo salama chini ya uongozi wa mwanasiasa huyo mkongwe.
Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ameeleza kukerwa na tetesi za mitandao ya jamii ilivyovumisha jina lake kuwa miongoni mwa wanaotajwa kuwa makamu mwenyekiti wa CCM (Bara).
“Sina budi kusema kwa sababu ya mitandao hii eeh! Wakati mwingine inakutoa jasho. Unafikiri labda kuna mmoja kanong’onezwa kwamba wewe mzee ndio unakwenda kuwa makamu, kumbe wapi, kumbe sivyo,” amesema.
Pinda aliyeongoza ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuangalia uchaguzi wa Botswana mwishoni mwa mwaka jana, amesema aliitwa na Rais Samia na wajumbe wenzake.
“Mimi ndio niliitwa wa kwanza nikaingia hapo, nikamsimulia mambo yalivyokwenda vizuri, mwishoni nikawa nimemaliza nikabaki namsikiliza ili aseme kama hii mitandao inavyoeneza, lakini hakufanyika hivyo.
“Lakini kumbe ndivyo ilivyo, sasa unataka akwambie siri halafu utoke uanze kuropoka? Hapana, kwa hiyo nimetoka mle, not so happy (siko na furaha hivyo), lakini nikasema angalau amenipa meseji,” amesema.
Amesema baada ya kutoka kwa Rais Samia akarudi kuangalia mitandao, akakuta minong’ono zaidi.
“Ukirudi mitandaoni, mama yangu mama yangu, waliona sijui nimepiga picha na nani, wakasema aah kumbe alikuwa ameitwa huko, nikawaambia aah, mngejua!”
Hata hivyo, baada ya kutajwa Wasira, Pinda amesema ameshukuru kwa kuwa mambo yameisha.
Akimzungumzia Wasira, amesema wamekuwa wakifungana katika minong’ono ya uteuzi, akirejea mwaka 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Lowassa kujiuzulu.
“Wala si kwamba unaambiwa omba fomu, hapana, mitandao tu ikaibuka na zake, Mizengo Pinda, Wasira, nani nani eh! Kila ukikutana na mzee mmoja atakumegea siri, hakuna hata mmoja, kwa hiyo na sasa limekuja limetokea leo,” amesema.
Pinda aliyefanya kazi na Wasira, amemwelezea kama mchapakazi na mwenye historia ya muda mrefu ya siasa tangu TANU mpaka CCM.
“Mimi sina shaka na uwezo wa huyu mzee hata kidogo, kwa sababu nimekuwa naye karibu ndani ya chama, hata tulipokuwa serikalini bado tumefanya kazi pamoja,” amesema.
Awali, akitoa azimio lililopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Dk Mohamed Said Dimwa amesema tabia, mwenendo na sifa za Wasira ndizo zilizosababisha halmashauri kuu ya chama hicho, kumteua awanie nafasi ya makamu mwenyekiti wa CCM (Bara).
“Halmashauri Kuu ya CCM, imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha pasipo shaka kuhusu tabia, mwenendo, tabia na sifa za mwanachama huyo kwa muda wote wa uhai ndani ya CCM.
“Pia, anazingatia kikamilifu masharti ya wanachama, sifa na miiko ya kiongozi kama ilivyoanishwa katika ibara ya 8, 17 na 18 za katiba ya CCM, daima amekuwa mstari wa mbele kupigania, kulinda masilahi ya chama chetu, umoja na mshikamano wa kitaifa.
“Ni mkweli, mnyenyekevu, anayependa nchi yake ni mtiifu ndani ya CCM na raia mwema,” amesema.
Rais Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM taifa amewaonya wanachama kujiepusha na makundi na kampeni za mapema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amewataka wana-CCM kuwa wamoja wanapoelekea katika uchaguzi mkuu.
“Tunawajibika kuondoka hapa tukiwa wamoja zaidi ili tukafanye maandalizi ya ushindi wetu wa 2025. Tuna wajibu wa kulinda uhuru wa nchi yetu, utu wetu na heshima ya wananchi wetu.
“Tutakapofika huko, safari itaanza muda si mrefu kuteua wagombea wanaokubalika na kutounda makundi. Tunasema makundi wakati wa kuomba kwa sababu ni demokrasia, waombaji watakuwa wengi kutakuwa na makundi mbalimbali.Tutakaposimamisha wagombea wa chama chetu tunaomba makundi yasiendelee,” ameonya.
Pia, amekemea kampeni za mapema zinazofanywa na baadhi ya makada wa chama hicho, wanaojipanga kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu unaokuja.
“Tayari tumepata malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanaofanya misafara kwenda majimboni, watu wanaoitisha mikutano mikuu ya majimbo kwa kisingizio cha ufugaji au mambo mengine, lakini lengo ni kujitambulisha kwa wanachama.Tunaushahidi wa picha nyingi sana, tunaomba kutoa onyo mapema,” amesema.
Amewaasa wana CCM kutoingiwa na kiburi cha kudharau wapinzani na pepo la kuwaogopa.
Samia amesema CCM ni chama kikubwa kimuundo, kioganaizesheni, kihistoria na hata kwa idadi ya wanachama.
Amesema hadi kufikia Desemba 31, 2024 CCM ilisajili wanachama zaidi ya milioni 12.1 kutoka wanachama milioni 3.96 waliokuwapo Mei 2021.
Katika kukiimarisha chama hicho, amesema kimenunua magari 194 yaliyosambazwa kwenye ofisi 149 za wilaya kati ya ofisi 198 sawa na asilimia 88.7.
“Tumetoa magari 32 kwa ofisi za CCM katika mikoa yote, vilevile tumetoa magari tisa yaani matatu kwa kila jumuiya za wazazi, UWT na UVCCM, ni shabaha yetu kuhakikisha wilaya 19 zilizobaki zinapata magari kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.
“Katika ngazi za kata, tumegawa manne kwa kila ofisi nchi nzima hadi Novemba 2024 tulikuwa tumekamilisha kazi kwa asilimia 100 nchi nzima,” amesema
Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Maendeleo (Tehama), amesema chama hicho kimekamilisha mradi maalumu wa kuunganisha mawasiliano kutoka makao makuu na kuwasiliana katika ngazi za mkoa na wilaya.