Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya wanachama wa chama hicho kujiepusha na makundi na kampeni za mapema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Samia amesema hayo leo Jumamosi Januari 18, 2025 katika mkutano mkuu wa CCM unaoendelea jijini Dodoma ukilenga kuziba nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho bara na kupata taarifa za utekelezaji wa ilani za uchaguzi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Amewataka wana CCM kuwa wamoja wanapoelekea katika uchaguzi mkuu.
“Tunawajibika kuondoka hapa tukiwa wamoja zaidi ili tukafanye maandalizi ya ushindi wetu wa 2025 tunawajibu wa kulinda uhuru wa nchi yetu, hadi ya utu wetu na heshima ya wananchi wetu.
“Tutakapofika huko, safari itaanza muda si mrefu kuteua wagombea wanaokubalika na kutounda makundi. Tunasema makundi wakati wa kuomba kwa sababu ni demokrasia, waombaji watakuwa wengi kutakuwa na makundi mbalimbali.
“Tutakaposimamisha wagombea wa chama chetu tunaomba makundi yasiendelee,” ameonya.
Pia, Rais Samia amekemea kampeni za mapema zinazofanywa na baadhi ya makada wa chama hicho, wanaojipanga kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu unaokuja.
“Tayari tayari, tayari, tumepata malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanaofanya misafara kwenda majimboni, watu wanaoitisha mikutano mikuu ya majimbo kwa kisingizio cha ufugaji au mambo mengine, lakini lengo ni kujitambulisha kwa wanachama.
“Tunaushahidi wa picha nyingi sana, tunaomba kutoa onyo mapema,”amesema.
Amewaasa wana CCM kutoingiwa na kiburi cha kudharau wapinzani na pepo la kuwaogopa. tupambane nao kulinda heshima tuliyopewa na wananchi katika kuliongoza Taifa letu.
Kuhusu ukubwa wa chama hicho, Samia amesema ni kikubwa kimuundo, kioganaizesheni, kihistoria na hata kwa idadi ya wanachama.
Amesema kufuatia usajili wa wanachama, hadi kufikia Desemba 31, 2024 CCM ilisajili wanachama zaidi ya milioni 12.1 kutoka wanachama milioni 3.96 hadi kufikia Mei 2021.
Katika kukiimarisha chama hicho, Samia amesema chama kimenunua magari 194 yaliyosambazwa kwenye ofisi 149 za wilaya kati ya ofisi 198 sawa na asilimia 88.7.
“Aidha tumetoa magari 32 kwa ofisi za CCM katika mikoa yote, vilevile tumetoa magari tisa yaani matatu kwa kila jumuiya za wazazi, UWT na UVCCM, ni shabaha yetu kuhakikisha wilaya 19 zilizobaki zinapata magari kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.
“Katika ngazi za kata na wadi, tumegawa manne kwa kila ofisi nchi nzima hadi Novemba 2024 tulikuwa tumekamilisha kazi kwa asilimia 100 nchi nzima,” amesema Samia.
Pia, amesema kwa kipindi cha mwaka 2022- 2024, chama kiliendesha mafunzo ya kiutendaji katika ngazi ya mkoa, wilaya, wadi hadi jimbo.
“Aidha tulipata mafunzo ndani na nje ya nchi katika ngazi mbalimbali na katika nje ya nchi tulikwenda sana China na India,” amesema.
Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Maendeleo (Tehama), amesema chama hicho kimekamilisha mradi maalumu wa kuunganisha mawasiliano kutoka makao makuu na kuwasiliana katika ngazi za mkoa na wilaya.