SERIKALI YAFANYA UTAFITI WA HALI YA UPATIKANAJI NA MATUMIZI YA NISHATI NCHINI

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inafanya utafiti wa tatu wa hali ya upatikanaji na matumizi ya nishati katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Hayo yameelezwa Januari 17, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Godfrey Chibulunje.

“Huu ni utafiti wa tatu kuwahi kufanywa na Wakala na hapa Serikali imelenga kubaini hali ya usambazaji na matumizi ya nishati ili kuboresha mipango yake katika sekta ya nishati kwa upana wake,” alisema Mha. Chibulunje.

Alisema ili kupata takwimu sahihi zenye uhalisia ambazo zitatumika kwenye uandaaji wa miradi ya usambazaji wa nishati mbalimbali ikiwemo ya umeme, kupikia na ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini; Wakala kwa kushirikiana na NBS wapo katika hatua ya ukusanyaji wa taarifa katika mikoa yote Tanzania Bara.

“Kwa sasa hatua inayoendelea kote nchini ni ukusanyaji wa taarifa ambao ni moja ya hatua muhimu katika utekelezaji wa tafiti hii,” alisema Mha. Chibulunje.

Mhandisi Chibulunje alisema katika tafiti ya pili iliyofanyika mwaka 2020 hali ya upatikanaji wa umeme vijijini ilikuwa ni asilimia 69.6.

Akizungumzia namna ambavyo zoezi hilo linafanyika kwa Mkoa wa Dodoma, Mratibu wa ukusanyaji wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Dodoma, Bi Nasriya Alli aliainisha namna ambavyo wanatekeleza tafiti hiyo mkoani humo kuanzia hatua ya kukutana na uongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji, kuainisha mipaka ya ukusanyaji wa takwimu na kaya zitakazohusika kwenye tafiti kama sampuli.

Zoezi hili la ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya tafiti ya upatikanaji na matumizi ya nishati ya kupikia na kuangazia lilianza tangu mwezi Desemba 2024 na linatarajia kuhitimishwa mwezi Januari 2025 ili kuendelea na uchakataji wa takwimu zilizokusanywa na Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kutoka mwezi Machi 2025.



Related Posts