Dar es Salaam. Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Sharifa Suleiman ameshinda nafasi ya uenyekiti wa baraza hilo atakaloliongoza kwa miaka mitano ijayo.
Sharifa ameshinda nafasi hiyo baada ya ushindi wa kura 222 katika uchaguzi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam leo Jumamosi Januari 18, 2025, dhidi ya kura 139 alizopata mshindani wake, Celestine Simba.
Hata hivyo, matokeo hayo yalikuwa ya duru ya pili ya uchaguzi huo, baada ya kurudiwa kutokana na kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.
Katika matokeo ya awali, Sharifa alipata kura 167, Celestine kura 116 na Suzan Kiwanga akiambulia kura 100.
Matokeo hayo, yalisababisha uchaguzi wa nafasi hiyo urudiwe kwa kuwa hakukuwa na mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.
Kabla ya nafasi hiyo, Sharifa alikuwa akikaimu wadhifa huo tangu mwaka 2020 baada ya aliyekuwa akiongoza nafasi hiyo, Halima Mdee na wenzake 18 kufukuzwa uanachama kwa kosa la usaliti.
Matokeo ya uchaguzi huo, yametangazwa leo, Jumamosi Januari 18, 2025 saa 8:30 usiku na Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Aida Kenani ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi mkoani Rukwa.
Kenani amesema uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bawacha ulikuwa na jumla ya wapiga kura 363, kati ya hizo halali zilikuwa 361 na mbili ziliharibika.
“Kwa mamlaka niliyopewa namtangaza Sharifa Suleiman kuwa Mwenyekiti wa Bawacha taifa,” amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wana-Chadema waliokuwepo ukumbini hapo.
Matokeo mengine aliyotangaza ni nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar na Wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu Bawacha.
Kenani amemtangaza Elizabeth Mwakimomo kuwa mshindi wa nafasi ya umakamu uenyekiti Bara, aliyepata kura 212 sawa na asilimia 59, huku mpinzani wake Salma Kasanzu akipata kura 147.
Hata matokeo hayo pia, amesema yalikuwa ya uchaguzi uliorudiwa baada ya awali kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50.