KIKOSI cha Simba kinaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kushuka uwanjani kukabiliana na CS Constantine ya Algeria katika mchezo wa Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikijaribu kupambana kukwepa mtego wa vigogo robo fainali.
Simba inahitaji ushindi katika mchezo wa kesho utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ili ijihakikishie uongozi wa kundi na ikitoka sare au kupoteza maana yake itabaki katika nafasi ya pili iliyopo sasa.
Kuna mambo mawili ambayo Simba itanufaika nayo ikimaliza katika nafasi ya kwanza katika kundi.
Kwanza itajihakikishia kumalizia nyumbani katika robo fainali kama kanuni ya mashindano inavyoeleza.
“Washindi wa pili watacheza mechi za kwanza za robo fainali nyumbani,” inafafanua kanuni ya 3(24) ya mashindano hayo.
Lakini jambo la pili ambalo Simba itapata ni kukwepa timu tatu tishio katika robo fainali ambazo zote kwa nyakati tofauti zimewahi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Timu tatu zinaongoza makundi mengine matatu ya mashindano hayo na mbili zimemaliza zikiwa vinara kwenye makundi huku moja ikiwa na nafasi kubwa ya kufanya hivyo.
Mbili zilizojihakikishia kuongoza makundi ni RS Berkane ya Morocco ambayo hata ikipoteza mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Stellenbosch itamaliza ikiwa kileleni mwa kundi B kwani ina pointi 13 na inayofuatia ina pointi tisa na pia kuna Zamalek ambayo imejihakikishia uongozi wa kundi D baada ya kukusanya pointi 11 huku inayofuatia ikiwa na pointi sita.
USM Alger ina nafasi kubwa ya kumaliza ikiwa kinara wa kundi C kwani ina pointi 11 na mechi ya mwisho itakuwa nyumbani ikicheza na ASC Jaraaf yenye pointi nane.
Zamalek imewahi kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili 2018/2019 na msimu uliopita wakati USM Alger ilitwaa mara moja 2022/2023.
RS Berkane imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara mbili – 2019/2020 na 2021/2022.
Ikumbukwe pia Simba katika mara tano tofauti ilizoshiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika, ni mara moja pekee ilimaliza ya kwanza kwenye kundi, hivyo msimu huu itakuwa ni mara ya pili ikiwa itafanikiwa kufanya hivyo.
Mara moja pekee ambayo Simba iliongoza kundi ni 2020/2021 ambapo ilikuwa ya kwanza kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika ikikusanya pointi 13 na nyuma yake kulikuwa na Al Ahly ikiwa na pointi 11.
Pambano la kesho limepewa mwamuzi kutoka Msumbiji, Celso Armindo Alvacao anayesifika kwa kumwaga kadi kama njugu, mbali na kutoa penalti.
Mwamuzi huyo atakayesaidiwa pia na waamuzi kutoka Msumbiji, ndio watakaoamua pambano hilo litakalofanyika kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Simba ikihitaji ushindi ili kumaliza kama kinara wa kundi hilo linaloongozwa kwa sasa na CS Constantine.
Alvacao ndiye atakayesimama kati kupuliza kipyenga na rekodi zinaonyesha mwamuzui huyo katika mechi 21 za kimataifa alizochezesha amemwaga jumla ya kadi 83 ikiwa ni wastani wa kadi 4 kwa kila mchezo, huku za njano zikiwa ni 81 na nyekundu mbili.
Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa na kismati na wenyeji kushinda kwani katika michezo hiyo 21, tisa timu wenyeji imeshinda, huku sita ikiwa ni kwa wageni kuibuka na ushindi na nyingine kama hizo zikiisha kwa sare.
Katika mechi tano zilizopita za kimataifa zikiwamo tatu za kufuzu za Afcon 2025 na mbili za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, ametoa jumla ya kadi za njano 15 kuonyesha, hana huruma kumwaga kadi kwa wachezaji wanaozingua uwanjani.
Simba kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 10, nyuma ya CS Constantine yenye 12 na zote zikiwa zimeshakata tiketi ya robo fainali, isipokuwa mchezo wa Jumapili ni wa kutaka kumaliza fitina baina yao nani awe kinara wa kundi na yupi amalize wa pili.
Kama Simba itamaliza ya pili kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na vigogo waliocheza fainali iliyopita ya michuano hiyo, RS Berkane ya Morocco au watetezi, Zamalek ya Misri kama sio mabingwa wa 2023, USM Alger ya Algeria zinazoongoza makundi ya B, C na D.
Iwapo Simba itamaliza kana kinara itavikwepa vigogo hivyo, lakini itaangukia mikononi mwa ama Stellenbosch ya Agfrika Kusini, Al Masry ya Misri kama sio Enyimba ya Nigeria au ASC Jaraaf ya Senegal au ASEC Mimosas ya Ivory Coast kutegemea na matokeo ya mechi za mwisho za makundi hayo matatu.
Simba imetinga hatua ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu mwaka 2018-2019, ikiwamo mbili za Shirikisho Afrika na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika.