Unguja. Baada ya kufungwa vifaa maalumu kwenye boti za wavuvi vya kuangalia masafa na kiwango cha samaki baharini (PDS), imeelezwa ufanisi waongezeka katika uvuvi.
Vifaa hivyo vinavyofungwa kwenye boti vinasaidia kutoa taarifa za wavuvi wanaokwenda baharini iwapo wakikumbwa na dhoruba au changamoto nyingine yoyote.
Mwenyekiti wa Kamati za Uvuvi kutoka Pemba, Sheha Abdalla Juma amesema mradi wa kufunga PDS umeleta tija kwa wavuvi kutokana na kupungua kwa upoteaji wa wavuvi wakiwa baharini.
Ametoa kauli hiyo leo Januari 18, 2025 wakati wa kikao kujadili utekelezaji na mwendelezo wa mradi huo kwa mwaka 2024/25.
Kikao hicho kinajadili mafanikio yaliyopatikana na namna ya kutatua changamoto zilizojitokeza katika mradi huo.
“Ni hatua kubwa baada ya kufunga vifaa hivi kweli tija ipo inaonekana. Matukio ya kupotea kwa wavuvi yamepungua, mvuvi anakwenda sehemu ambayo kuna samaki siyo kwenda ilimradi anakwenda baharini,” amesema.
Hata hivyo, hakubainisha matukio ya kabla na baada ya kufunga vifaa hivyo.
Ametumia fursa hiyo kuziomba mamlaka husika kuongeza vifaa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na mradi huo ili kufikia malengo yaliokusudiwa na Serikali.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, Dk Salum Soud Hamed amewataka wavuvi kuendelea kutoa ushirikiano wa pamoja juu ya utunzaji wa vifaa hivyo ili kuleta mabadiliko ya uvuvi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari, Dk Zakaria Ali Khamis amesema iwapo vifaa hivyo vikitunzwa na kutumiwa katika misingi inayotakiwa, vitaleta mabdiliko makubwa katika sekta ya uvuvi.
Msimamizi wa mradi huo, Prisca John kutoka Shirika la World Fish amesema umelenga kutoa mafunzo ya uchukuaji wa takwimu katika maeneo yalifikiwa ili kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
“Hii inasaidia kupata taarifa za kila tukio ambazo ni sahihi na zinapatikana kwa wakati,” amesema.