Wanufaika wa Tasaf Mwanza waanzisha vizimba vya samaki

Mwanza. Jumla ya Sh34 milioni zimetumika kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki katika vizimba utakaonufaisha kaya 27 zilizopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika Mtaa wa Kayenze Ndogo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akitoa taarifa ya mradi huo kwa wajumbe wa uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kitaifa walioutembelea kuukagua, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kayenze Ndogo, George Ndimi amesema wanufaika hao watavuna samaki wenye thamani ya Sh31.2 milioni kila awamu ndani ya miaka mitano.

“Lengo kuu la mradi ni kuongeza kipato cha wanakaya 27 waliopo katika vikundi viwili vya Temeke chenye wanachama 15 na Maliganya chenye wanachama 12.

“Mradi ulianza kutekelezwa Julai, 2024 kwa kufanya ununuzi wa vizimba, vifaranga na chakula cha samaki kwa hatua tofauti za ukuaji,” amesema Ndimi.

 “Mradi huu unafuga samaki 13,000 na kila kizimba kina samaki wa 6,500 aina ya sato. Samaki 13,000 waliopo kwenye vizimba hivi walipandikizwa Novemba 13, 2024 na wanategemea kukua kufikisha uzito wa  gramu 350 kwa miezi tisa, Hivyo uvunaji wa samaki utafanyika Julai, 2025,” amesema.

Amesema kipato cha Sh31.2 milioni kitapatikana baada ya kuuzwa kwa bei ya wastani wa Sh7,200 kwa kilo moja ya samaki iliyopo sokoni kwa sasa.

“Soko la samaki wa sato ni la uhakika, maana uhitaji ni mkubwa na inakadiriwa mauzo ya samaki wote yatafanyika kwa siku moja hadi mbili. Pia, mauzo yatafanyika eneo la mradi, hivyo hakutakuwa na gharama ya kupeleka mzigo sokoni wala muda kutumika kuuza samaki hao,” ameeleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ufugaji Samaki (Sameki), Said Meck Sadick amewataka vijana na wanufaika wengine wa mpango huo kuchangamkia fursa ya ufugaji samaki, akisema unalipa na kuna uhitaji mkubwa wa kitoweo hicho kwa walaji.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, mjumbe wa uongozi wa kitaifa wa Tasaf, Dk Naftali Ng’ondi ameishukuru kampuni hiyo kwa kusimamia shuguli za uzalishaji wa samaki hao pamoja na kutoa wataalamu wanaowafundisha wanufaika hao njia nzuri za kufuga na kupata mazao mengi.

Related Posts