Wasira aanza kazi na mambo mawili

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kwa kumchagua, huku akisema anaianza kazi hiyo kwa kuhakikisha chama kinaendelea kushinda  katika uchaguzi na kushika dola.

Pia, amesema atahakikisha anasimamia umoja, amani na maendeleo.

Wasira amesema hayo leo Januari 18, 2025 katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma, baada ya jina lake kutajwa na kupigiwa kura.

“Kazi ya chama hiki imeelezwa kwenye ibara ya 5 ya Katiba ya CCM, ambayo ni kushinda uchaguzi kukamata dola ya ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar na Serikali za mitaa,” amesema.

Amesema kwa sasa wameshashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, lakini bado kazi iko mbele.

“Sasa kazi tulitonayo ni kukamata dola ya Jamhuri ya Muungano na Jamhuri ya Zanzibar. Ndugu zangu Waislamu wanasema kanzu ya Ijumaa inafuliwa Alhamisi, sasa hivi wamebadilisha wanasema tufue Jumatano, sasa Jumatano imeshapita tumechukua Serikali za mitaa.

“Sasa tujiandae ikifika Oktoba kazi ya kuchukua dola inakamilika,” amesema.

Amesema ili kushinda watajinadi kwa kueleza utekelezaji wa ahadi walizotoa.

“Tumejenga shule kila mahali, tunatua ndoo kina mama kichwani kila mahali, halafu miradi ya maendeleo tuliyoambiwa baada ya Rais John Magufuli kututoka akakabidhiwa Samia, sasa reli mpaka Dodoma na reli ile ina makandarasi mpaka Kigoma.

“Kuna daraja linaitwa la Magufuli kule Busisi (Mwanza) linakamilika, kuna bwawa la umeme linakamilika, kama hivyo ndivyo twendeni tukashinde basi, maana sababu za kushinda zipo, nia ipo na uwezo tunao,” amesema.

Kazi ya pili aliyosema anaitekeleza ni kutangaza kwa dunia na Watanzania wajue kwamba CCM ni chama cha amani ni chama cha maendeleo.

“Ndio ajenda zetu, tunapewa nchi ili tufanye maendeleo, lakini huwezi kufanya maendeleo bila amani, maana amani ndio msingi wa maendeleo,” amesema.

Wasira aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua na wale ambao hawakumchagua.

Pia, amemshukuru mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuteua jina lake na hatimaye wajumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu kulipitisha kabla ya kwenda mkutano mkuu.

Related Posts