Watumishi Mwanza kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa mazoezi

Mwanza. Mkoa wa Mwanza umeanzisha kampeni ya watumishi wa umma ya kufanya mazoezi ya viungo kila Jumamosi ya tatu ya mwezi ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo Jumamosi Januari 18, 2025 kwa kutembea na kukimbia kilomita tano.

Katibu tawala msaidizi- Miundombinu, Chagu  Ng’oma amesema kwa miaka mitano magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kwa asilimia 65.5 kutoka wagonjwa 149,130 mwaka 2020 hadi 224,190 mwaka 2024.

Amesema magonjwa hayo yanachangia kupunguza ufanisi wa utendaji kazi katika utumishi wa umma, lakini mazoezi ya viungo, mtindo wa maisha na ulaji unaofaa vitazuia magonjwa ya moyo na kisukari kwa asilimia 80 na saratani kwa asilimia 50.

Ng’oma amesema udhibiti wa magonjwa hayo mahala pa kazi unahitaji msukumo wa kipekee ili kunusuru afya zao, ndiyo maana wamekuja na mazoezi hayo ambayo ni ya lazima na endelevu ili kudumisha afya bora kwa watumishi wa umma.

“Tatizo la magonjwa sugu yasiyoambukiza limebainika kuathiri afya za watumishi kwa kiwango kikubwa na kupungua kwa nguvu kazi kutokana na vifo, kuongezeka kwa gharama za matibabu na kupungua kwa tija kazini, hivyo kuathiri ukuaji wa pato la Taifa,” amesema Ng’oma.

Baadhi ya watumishi wa umma katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakifanya mazoezi ya viungo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya hiari ya mazoezi kwa watumishi wa umma itakayokuwa ikifanyika kila Jumamosi ya tatu ya mwezi ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza. Picha na Damian Masyenene

 “Mbinu za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza zinajulikana na zipo ndani ya uwezo wetu watumishi kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha na ulaji unaofaa, mazoezi ya mwili na kuwa na uzito usiozidi kiasi.”

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mashauri amesema zaidi ya asilimia 50 ya watumishi wa umma wana viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza huku kisukari na shinikizo la damu yakiongoza.

“Tatizo hili kwa Mkoa wa Mwanza miaka mitano iliyopita limeongezeka hadi asilimia 8.1 mwaka 2024 kutoka asilimia 6.4 mwaka 2020. Mpango huu utaendeleza juhudi za watumishi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ambukiza,” amesema Mashauri.

Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Mwanza, Dk Saula Beichumila amesema utaratibu huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa mikoa yote nchini kutokana na kuongezeka kwa magonjwa hayo.

Mmoja wa watumishi wa umma aliyeshiriki mazoezi hayo, Samson Neligwa amesema utaratibu huo ni mzuri kwa kuwa watumishi wengi wanaosumbuliwa na magonjwa hayo wanapokwenda kutibiwa wanashauriwa kufanya mazoezi.

“Kufanya mazoezi ukiwa peke yako huwa kuna uzito, lakini haya mazoezi ya ujumuishi yanatupa morali hata wale ambao ni wavivu watahamasika. Nawashauri watumishi wenzetu ambao hawajahudhuria leo wajitahidi kuja awamu ijayo ili kuongeza morali ya kupenda mazoezi,” amesema Neligwa.

Josepha Tarimo, Ofisa Ugavi Mwandamizi Mkoa wa Mwanza, amesema: “Watumishi wengi tunashinda ofisini, hatuna muda wa kufanya mazoezi ukishatoka ofisini unarudi nyumbani unakokutana na majukumu mengine, hivyo, huu utaratibu utatusaidia sisi tunaoshinda ofisini.”

Related Posts