KOCHA wa Yanga, Sead Ramovic ameamua kuiwekea MC Alger kikosi cha maangamizi akianza na washambuliaji watatu ambao wamekuwa wapo vizuri katika kucheka na nyavu na kusaidia mashambulizi.
Muda mchache ujao, Yanga itashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuvaana na wageni wao kutoka Algeria katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga yenye pointi saba, inahitaji ushindi ili kufikisha 10 na kuipiku MC Alger inayokamata nafasi ya pili na pointi zake nane. Vinara Al Hilal wameshafuzu robo fainali baada ya kufikisha pointi 10 na wana uhakika wa kumaliza nafasi hiyo hata wakipoteza mechi ya mwisho kwa TP Mazembe inayoburuza mkia na haina nafasi ya kwenda robo fainali.
Ramovic ambaye anasaka ushindi wa lazima leo ili kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi chake cha kwanza amewasimamisha washambuliaji watatu Prince Dube, Clement Mzize na Kennedy Musonda.
Hii ni mara ya kwanza kwa washambuliaji hao watatu kuanza pamoja msimu huu jambo linaloashiria Ramovic anataka kufunga mabao mengi leo.
Rekodi zinaonyesha katika mabao 22 ambayo Yanga imefunga kimataifa msimu huu kuanzia mtoano hadi sasa makundi, washambuliaji hao watatu jumla wamefunga nane ambapo Dube na Mzize kila mmoja ana manne wakati Musonda bado hajafunga.
Ukiweka kando rekodi hizo za kimataifa, washambuliaji hao pia wamefunga katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Mzize akiwa nayo sita, Dube (5) na hat trick moja wakati Musonda amefunga mawili. Jumla Yanga ina mabao 32 kwenye ligi washambuliaji hao wakiwa nayo 13.
Uzuri wa Musonda na Mzize, wana uwezo wa kutokea pembeni wakiwa na kasi jambo ambalo walinzi wa MC Alger wanaweza kuwa kwenye wakati mgumu zaidi huku Dube akisimamishwa kama mshambuliaji kinara pale mbele.
Kikosi cha Yanga kinachoanza kipo hivi; Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki na Kennedy Musonda.
Benchi wapo Aboutwalib Mshery, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Duke Abuya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shekhan Khamis, Clatous Chama na Pacome Zouzoua.