YANGA imeshindwa kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya jioni hii kulazimishwa suluhu na MC Alger ya Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo inayonolewa na Mjerumani, Saed Ramovic ilihitaji ushindi wa aina yoyote ile ili ifuzu tena robo fainali kama ilivyofanya msimu uliopita ilipokuwa chini ya kocha Miguel Gamondi aliyetimuliwa mara alipoiwezesha timu hiyo kutinga makundi ya michuano ya msimu huu.
Yanga iliyokuwa na pointi saba ilihitaji ushindi ili kufikisha pointi 10 ambazo zingeifanya kuungana na Al Hilal ya Sudan iliyoongoza kundi A ikiwa na pointi 10 baada ya jioni hii imepasuliwa ugenini kwa mabao 4-0 na TP Mazembe ya DR Congo, huku MC Alger ikifikisha pointi tisa na kukata tiketi ya kucheza robo.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikuwa za kimkakati kwa timu zote mbili zilikuwa zinashambuliana kwa zamu huku Yanga ikitawala zaidi mchezo huo tofauti na wapinzani wao.
Yanga iliyoanza na washambuliaji wawili, Kennedy Musonda na Prince Dube, ilianza kwa kutengeneza mashambulizi ya kusaka bao la utangulizi ambapo dakika ya 11 tu, Stephane Aziz KI alishindwa kuuzamisha mpira wavuni baada ya shuti lake kuokolewa na kipa wa MC Alger, Abdelatif Ramdane.
Hata hivyo, licha ya MC Alger kuhitaji sare tu ili ifuzu hatua ya robo fainali ila haikuwa kinyonge kwani ilishambulia pia kwa kushtukiza huku dakika ya 23, nyota wa timu hiyo, Akram Bouras alishindwa kuzamisha mpira wavuni akiwa eneo la 18, baada ya shuti lake kuokolewa na beki, Ibrahim Bacca.
Wakati Yanga ikitengeneza mashambulizi ya kusaka bao la utangulizi, kwa upande wa wapinzani wao kuanza mbinu za kupoteza muda mapema tu baada ya kujiangusha chini mara kwa mara kwa lengo la kupunguza presha iliyokuwa inawakabili na kuiweza kuibana Yanga hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika suluhu.
Kipindi cha pili timu zote zilianza kwa kufanya mabadiliko ambapo Yanga ilimtoa Kennedy Musonda ambaye tangu mwanzoni alishindwa kuonekana na nafasi yake kuchukuliwa na Pacome Zouzoua ili kuongeza kasi eneo la ushambuliaji.
Pia kitendo cha kuingia Clatous Chama na kutoka Mudathir Yahya, kilionyesha Yanga ilihitaji mtu atakayeweza kuamua mchezo kutokana na rekodi za ‘Mwamba huyo wa Lusaka’ alizonazo katika michuano ya kimataifa.
Kwa upande wa MC Alger ilijibu pia mapigo kwa kuingiza washambuliaji wawili, Zakaria Naidji na Andy Delort na kuzifanya timu zote kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara.
Suluhu ya leo imeifanya Yanga kuendeleza uteja mbele ya MC Alger baada mchezo wa kwanza uliopigwa Algeria kuchapwa mabao 2-0, Desemba 7, mwaka jana.
Huu ni mchezo wa nne kwa timu hizi kukutana ambapo mara ya kwanza zilianza kukutana Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam Yanga ilishinda bao 1-0, Aprili 8, 2017, kisha marudiano kuchapwa mabao 4-0, Aprili 15, 2017.,
Achana na bao la Mama ambalo huwa linatolewa ikiwa timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho Afrika inazipata ikipata ushindi ila kitendo cha Yanga kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali imeinyima klabu hiyo kitita cha Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni) ambazo kila timu inayofikia hatua hiyo inakuwa na uhakika wa kupata kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).
Katika mchezo Yanga ilitawala mchezo huo kwa asilimia 68 dhidi ya 32 za wageni, ikipiga kona 14 dhidi ya moja ya wageni, huku ikifanya mashambulizi 18 na kupiga mashuti 11, matatu yakilenga lango na nane yakienda kombo, wakati MC Alger ilipiga jumla ya mashuti matatu tu, moja likilenga lango na mengine mawili yakienda kando katika mashambulizi matatu iliyofanya.
Kwa sasa Yanga inarudi kujiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Copco ya Mwanza katika hatua ya 64 Bora sambamba na kusubiri kuanza kwa ngwe ya pili ya Ligi Kuu Bara ikianza na kiporo dhidi ya Kagera Sugar, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex.
YANGA: Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Khalid Aucho, Stephane Aziz KI, Clement Mzize, Mudathir Yahya/ Clatous Chama, Kennedy Musonda/ Pacome Zouzoua, Prince Dube.
MC Alger: Abdelatif Ramdane, Ayoub Abdellaoui, Mohamed Benkhemassa/Andy Delort, Soufiane Bayazid/Hamza Mouali, Tayeb Meziani/Zakaria Naidji, Kamel Hamidi, Ayoub Ghezala, Mohammed Reda Halaimia, Larbi Tabti/Zakaria Draoui, Amine Ben Malik Messoussa, Akram Bouras/Abdelkader Menezla.