Swali: Mume wa mtu ananihudumia na kunijali mpaka natamani awe mume wangu. Huu mwaka wa tatu nipo naye, naomba mbinu ili afikirie kunioa, kwani pamoja na kunijali hajawahi hata siku moja kuzungumzia kufunga ndoa na mimi.
Ndiyo najua ameoa, tena kanisani, ila angalau angenitania nijue kuwa ipo siku tunaweza kufanya maarifa ya kuoana. Hakika ninampenda na ninajua ananipenda sana pia.
Jibu: Duh! Sijui niseme una uvivu wa kufikiri au niseme umekosa maadili tu! Unawezaje kutamani kuolewa na mwanamume ambaye ana ndoa na unatambua kabisa imani yake ya kidini inatambua ndoa ya mke mmoja.
Hata akijadili au kuzungumzia suala hilo kama unavyotamani unadhani litakuwa na maana, ilhali unatambua wazi hawezi kuoa zaidi ya mke mmoja?
Jitulize na utulize akili ufikirie kwa kina utagundua umeamua kupoteza muda kwa kumtumikia mumeo wa mwenzako kwa maana ya kumpa kila atakacho, kisha anarudi kwa mkewe.
Matamanio haya yanaonyesha dhahiri kukosekana kwa maadili.
Kuwaza kuolewa na mume wa mtu mwingine ni kama kuwekeza katika mradi usiotabirika. Ni kama kuandika hadithi ambayo kwa kawaida haina furaha.
Naam! Haina furaha kwa sababu mwisho wa siku hata akae na wewe miaka 10 atabaki kuwa mume wa mtu tu na si wa kwako.
Utakachofanikiwa ni kumtenganisha na mkewe na watoto wake kama anao na kujipatia laana zao kila wanapokosa mapenzi ya mzazi wao, pia kumfanya aonekane hana adabu mbele ya jamii, tofauti na hapo hakuna furaha ya kudumu.
Ni rahisi kupoteza heshima na hadhi katika jamii kutokana na hatua kama hizi.
Ni muhimu kuelewa kuwa upendo wa kweli hauwezi kuanzishwa kwenye msingi wa mahusiano yaliyovunjika.
Hata ukiolewa baada ya kupambana ili amuache mkewe unadhani utakuwa na ndoa ya furaha au utalazimika kuilazimisha furaha? Jitahidi kufikiria mara mbili huku ukiushinda moyo wa kuomba kuolewa na mume wa mtu.
Unapoamua kusonga mbele katika uhusiano wa aina hii, unapaswa kutafakari juu ya madhara na kujaribu kuelewa ni vipi hatua zao zitaweza kuwadhuru sio tu watu wengine, bali pia nafsi zao wenyewe.
Kwa jumla, tamaa ya kuolewa na mume wa mtu si tu ni hatari, bali pia ni kinyume na maadili ya msingi ya upendo na heshima. Kila mmoja anapaswa kujifunza kuheshimu ndoa ya wengine na kutafuta furaha katika mahusiano ambayo hayana migongano.
Ila na nyinyi wanaume huwa mnatafuta nini. Au basi.
Aliyenipa mimba kaikataa, niitoe?
Swali: Nina mimba ya miezi minne, aliyenipa ameikataa, natamani kuitoa. Marafiki zangu wanasema niitoe, naomba ushauri wapi ninaweza kuitoa salama bila kupata madhara?
Jibu: Karibu kwa maswali ya kujenga, hili halina mashiko, yaani unanishirikisha katika mawazo yako hasi ya kutaka kukidhuru kiumbe kisicho na hatia?
Nilitamani nisikujibu kabisa, ila nakujibu kwa faida ya wengine, ukibeba mimba tambua umebeba mtoto wako na unazaa kwa faida yako.
Kama una mwenza wako ni sawa, ila ikikataliwa suluhisho siyo kuitoa, bali ni kujipanga kulea mtoto.
Siku nyingine kabla hujaingia kwenye ngono zembe fikiria kuhusu mimba, unapanda mahindi unataka uvune kande? Achana na habari ya kutoa hiyo mimba. Kama haupo tayari kuzaa tumia kinga.
Nakutia moyo hakuna kitakachoshindikana, hata kama utapata taabu kiasi gani lazima mtoto akue na kwa taarifa yako atakuwa na akili, upendo, msikivu na Mungu atamuepusha na maradhi ili iwe rahisi kumlea. Sema Amina na usonge mbele kulea mimba.