Bila ya mashabiki, Simba yamzima Mwarabu

SIMBA imetoa darasa tamu kwa watani wao wa jadi, Yanga baada ya jioni ya leo kushinda mabao 2-0 mbele ya CS Constantine ya Algeria, licha ya kucheza bila ya mashabiki kutokana na kutumikia adhabu iliyopewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ambao ukikuwa na maofisa wa timu hizo mbili na wale wa CAF sambamba na wanahabari kutokana klabu hiyo ya Msimbazi kufungiwa na CAF kuingiza mashabiki kwa kosa lililotokea katika mchezo wao dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Ushindi huo umeifanya Simba inamalize mechi za makundi ikiwa kinara wa Kundi A katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiizidi ujanja Constantine iliyosalia na pointi 12, huku Bravos do Maquis ya Angola iliyofumuliwa 4-0 na CS Sfaxien ya Tunisia ikibaki ya tatu na pointi saba. Sfaxien ambayo nido mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa michuano ya Kombe la Washindi na lile la CAF, ikisalia mkiani ikiwa na pointi tatu.

Simba ililazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kuweza kuandika mabao hayo, baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika bila timu yoyote kupata bao, licha ya kushambuliana kwa zamu na kutengeneza nafasi kadhaa zilizopotezwa na wachezaji wa timu zote mbili.

Constantine iliingia kipindi cha pili ikifanya badiliko la kumtoa mshambiliaji Mingeria, Tosin Omoyele na kumuingiza Abdennour Belhocini, lakini haikuizuia Simba kuandika bao la kwanza dakika ya 61 lililofungwa na Kibu Denis aliyemalizia pasi tamu ya nyota mpya wa kikosi hicho, Ellie Mpanzu aliyemgongea vizuri kabla ya mfungaji kufumua shuti kali lililomshinda nguvu kipa wa Constantine, Zakaria Bouhalfaya.

Baada ya bao hilo wageni walifanya mabadiliko mengine ya wachezaji watatu, lakini ikawa ni kama mwiba kwao kwani walijikuta wakifungwa bao jingine la pili lililowekwa kimiani na Leonel Ateba dakika ya 79 akimalizia krosi ya chini ya beki wa kulia Shomari Kapombe. Hilo lilikuwa ni bao la pili kwa Atebam lakini Kibu akifikisha matatu katika mechi sita walizocheza.

Baada ya mabao hayo, kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya wachezaji watano kwa kuwatoa Fabrice Ngoma, Jean Ahoua, Mohammed Hussein, Atena na Yusuf Kagoma na kuwaingiza Debora Mavambo, Ladack Chasambi, Valentin Nouma, Edwin Balua, Mzamiru Yassin na kuwabana wageni.

Matokeo hayo yameifanya Simba kulipa kisasi cha kipigo ilichopewa katika mchezo wa kwanza dhidi ya CS Constantine walipowafumua 2-1 mjini Constantine, Algeria, lakini imeiwezesha sasa kuwa na hakika ya kutokutana na vigogo watatu wa michuano hiyo, watetezi Zamalek ya Misri, USM Alger ya Algeria au RS Berkane ya Morocco ambao nao wamemaliza kama vinara wa makundi ya B, C na D.

Simba inayosubiri droo ya hatua hiyo ya robo fainali kujua itakutana na timu ipi kati ya Stellenbosch ya Afrika Kusini iliyomaliza ya pili katika Kundi B, Jaaraaf ya Senegal au ASEC Mimosas ya Ivory Coast zilizopo Kundi C ama Al Masry ya Misri au Enyimba ya Nigeria ambazo zinatarajia kushuka uwanjani usiku huu kukamilisha ratiba ya mechi za hatua hiyo ya makundi ili kuungana na vigogo vilivyotangulia mapema hatua hiyo.

Katika mchezo wa leo, Simba ilicheza bila mashabiki kutokana na kufungiwa na CAF kwa kosa la fujo zilizotokea ilipoumana na Sfaxien, lakini haikuizuia timu hiyo kucheza kwa bidii, huku mashabiki hao wakijazana viwanja vya Mwembe Yanga walipowekewa runinga kubwa kuangalia mchezo huo.

Related Posts