Dar es Salaam. Ukiachana na makali ya maisha katika kila Januari, hekaheka za siasa ni jambo jipya lililoukabili mwezi huo tangu ulipoanza mwaka 2025.
Hilo linatokana na matukio mbalimbali yanayofanywa na vyama maarufu vya siasa nchini vya ACT-Wazalendo, Chadema na CCM tangu ulipoanza mwezi Januari.
Ni mwezi wa hekaheka katika siasa, kwa sababu chama kikuu cha upinzani Chadema, kinafanya uchaguzi wake wa ndani, unaohusisha nafasi za kitaifa za mabaraza na chama kwa ujumla wake.
Uchaguzi pekee pengine isingekuwa hekaheka, lakini uamuzi wa viongozi wawili waandamizi ndani ya chama hicho, kutangaza nia ya kugombea uenyekiti wa taifa, ni hekaheka tosha.
Makada hao ni Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo aliyoishika kwa miaka 21 na anashindana na makamu wake bara, Tundu Lissu.
Ushawishi wa kisiasa walionao wawili hao, umesababisha hata chaguzi za mabaraza ya chama hicho, zifanyike kwa sura ya kati ya wanaomuunga mkono Lissu na wale wa Mbowe.
Uwanja wa mapambano wa wagombea hao ni ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na siku ya hukumu ni Jumanne ya Januari 21, 2025, hii nayo ni siku ya hekaheka.
Wakati ya Chadema yakiendelea hivyo, chama tawala nacho CCM, kinaendelea na mkutano mkuu wa kitaifa ulioanza jana Jumamosi na unahitimishwa leo Jumapili.
Januari inabaki kuwa mwezi wa hekaheka za kisiasa, hasa ukizingatia mkutano mkuu huo wa CCM umehusisha uchaguzi uliomua kupatikana kwa mrithi wa Abdulrahman Kinana aliyekuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho bara.
Majina mbalimbali ya wanasiasa wakongwe wakiwamo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge mstaafu Anna Makinda na waziri mwandamizi mstaafu Stephen Wasira yalikuwa yakitajwa zaidi.
Mwisho ya wote ni kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho ikampendekeza Wasira mbele ya mkutano mkuu huo jana Jumamosi na kupigiwa kura 1,910 sawa na asilimia 99 na sasa ndiye Makamu mwenyekiti bara.
Kwa upande wa Chama cha ACT-Wazalendo, hekaheka zinakuja baada ya hatua yake ya kufungua pazia kwa wanachama wake, kujitokeza kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hatua hiyo, inakifanya ACT-Wazalendo kuwa chama cha kwanza cha siasa, kutangaza fursa hiyo kwa wanachama wake, huku vingine vikiendelea na harakati za maandalizi.
“ACT-Wazalendo kinawatangazia Watanzania mchakato wa kutangaza nia za kugombea urais, ubunge na udiwani umefunguliwa leo Januari 15, 2025 (juzi).
Tamko hili ni utekelezaji wa azimio la Halmashauri Kuu ya ACT-Wazalendo iliyoagiza chama kiweke utaratibu na kuratibu utangazaji wa nia wa nafasi hizo,” alisema Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu.
Hata hivyo, wadau wa siasa wanaonya kuzingatiwa kwa miongozo na Katiba za vyama husika, ili kuhakikisha vinaivuka Januari salama.
Tayari Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu ameweka nia ya kuwania urais wa Tanzania huku Mwenyekiti wa chama hicho, Othuman Masoud ameweka nia kama hiyo upande wa Zanzibar.
Othman ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar jana Jumamosi amezindua timu ya ushindi kwenye harakati zake hizo.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza alibainisha mambo 10 yenye tafakuri tunduizi na hatima ya vyama vya siasa kwa hekaheka zake za Januari.
Aliandika yapo mambo kadhaa inabidi yaongoze fikra za wanachama wa vyama hivyo lakini pia Watanzania kwa ujumla kwa sababu, vyama hivi vimeshikilia sarafu ya Watanzania kwenye tundu la choo.
Alisema Chadema ina mashabiki wengi kuliko wanachama. Itafanya kosa kubwa kufikiri mawazo ya viongozi ndiyo ya wanachama na mashabiki.
Pia, alieleza CCM ina wanachama wengi kuliko mashabiki. Itafanya makosa makubwa kufikiri mawazo ya wanachama wake ndiyo mawazo ya nchi.
“Mbele ya CCM, CDM kinaonekana kama shetani aliyebeba habari njema. Ndiyo maana kada wa CDM akihamia CCM anapewa uongozi bila semina elekezi.
Mbele ya CDM, CCM kinaonekana kama malaika aliyebeba habari mbaya. CDM wanaona CCM ina fursa zisizotumika kubadili maisha ya watu. Ndiyo maana CDM inakazana na agenda mpya (katiba mpya, uhuru wa tume za uchaguzi),” alisema.
Askofu Bagonza anaendelea kueleza kuwa, agenda ya mabadiliko katika chaguzi na mikutano ya CDM na CCM mwezi huu wa Januari 2025, inavichanganya vyama vyote. Mabadiliko ni tishio na ni fursa.
Anaeleza, mashabiki na wanachama wa CDM wanaelekea kuchagua mabadiliko hata kama yatakiua chama kwa tumaini la ufufuko. Masikio yasiyosikia sauti hizi hayahitaji dawa. Tumaini la ufufuko ni gumu lakini ni msingi wa dini fulani inayoheshimiwa hata na wanaoipinga.
Katika andiko hilo aliloliweka kwenye mitandao ya kijamii, Bagonza anaendelea kufafanua kuwa, viongozi wengi wa CDM wanaelekea kutafakari tishio la mabadiliko kuliko fursa ya mabadiliko. Wanasema “Shetani uliyemzoea ni bora kuliko malaika wa ahadi.” Tishio la kumpoteza ‘shetani’ na wasimpate ‘malaika’ linawatafuna.
Anaeleza, CCM inauwazia uchaguzi wa CDM kuliko uchaguzi wa Makamu wake. Watanzania huichagulia CCM Mwenyekiti na kisha Mwenyekiti huyo huichagulia CCM Makamu wake. Wajumbe wanaenda Dodoma kukagua maendeleo ya jiji la Dodoma. Kimsingi, Makamu Mwenyekiti wa CCM ndiye Mwenyekiti ‘kivuli’ CCM ili kumpa ‘Mwenyekiti-Rais’ nafasi ya kuongoza nchi. Kwa hiyo CCM na CDM wanachagua wenyeviti mwezi huu.
Bagonza anaeleza, wagombea wa CDM wamekaa kwa ‘uzembe wa kimkakati’. Hii timu Lisu/Heche dhidi ya timu Mbowe/Wenje ni kama mtego wa panya. Matokeo yakiwa Lisu/Wenje au Mbowe/Heche, demokrasia itaingia majaribuni. Bahati mbaya, ni rahisi kuingia mbinguni kuliko kusajili chama kipya Tanzania.
“Ukweli mchungu: CCM inaihitaji CDM imara kuliko inavyolihitaji kundi moja ndani ya CDM. CDM dhaifu ni sumu ya CCM. Na CDM inayahitaji mawazo ya mashabiki kuliko ya viongozi. Taifa imara linaihitaji CCM na CDM imara. CCM acheni kiburi na CDM acheni utoto,”anaeleza Askofu Bagonza kwenye andiko hilo.
Anaeleza, palipoandikwa CDM unaweza kuweka ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi n.k na maana itabaki ileile. “Palipoandikwa CCM ondoa Polisi mawazoni mwako ibaki CCM peke yake.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Dk Lazaro Swai alisema hekaheka zinaweza kuja na athari au faida chanya kwa vyama vya siasa.
Athari zinatokana na kile alichoeleza, katika nyakati kama hizi, vyama vya siasa aghalabu hukacha misingi yake na kuamua kutenda vitu kwa mazoea.
Alisema katika kipindi ambacho mwamko wa uelewa wa wanachama kuhusu katiba za vyama vyao ni mkubwa, muhimu kila chama kienende kwa kuzingatia misingi hiyo.
“Huu ni wakati muhimu wa vyama kuzingatia misingi iliyovifanya viwepo, vikue na kuwa na majina viliyonayo.
“Vinapaswa kuzingatia misingi ya katiba zao, na mara nyingi tatizo katika nyakati kama hizi vyama vinasahau kufuata misingi ya katiba vinafanya kazi kwa mazoea,” alieleza.
Iwapo vyama vinaingia kwenye hekaheka zilizopo bila kuzingatia misingi yake, alisema kuna hatari vikapoteza kabisa nguvu yake na kugawanyika.
“Hekaheka zinaonekana nyingi nyakati hizi, lakini kama kuna chama kitazingatia misingi yake, vitafika pamoja na kuwa na nguvu kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema.