Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewapitisha makada wake 23 kuwania ujumbe wa Kamati Kuu.
Hatua ya kupitishwa kwa wagombea hao, imekuja baada ya leo, Jumapili Januari 19, 2025 kusailiwa katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema imeweka wazi wagombea hao wamepitishwa na kamati kuu iliyoketi leo.
Taarifa hiyo imewataja wagombea wanaume waliopitishwa kwa upande wa bara ni Bashir Abdallah Selemani na Daniel Ngogo.
Wengine ni John Pambalu, Nyamatari Tengecha, Patrick Sosopi, Patrick Assenga, General Kaduma na William Mungai.
Kwa upande wa nafasi za wanawake bara, imeeleza ni Dorcas Mwilafi, Ema Boki, Grace Kiwelu, Josephine Lemoyan, Monica Nsaro, Pasquina Lucas, Rehema Mkoha na Sina Manzi.
Katika nafasi za watu weye ulemavu, taarifa imeeleza wamepitishwa Salum Barwani, Amina Sollah na Sara Katanga.
Kwa upande wa nafasi za wanawake Zanzibar waliopitishwa ni Time Suleiman,
Zeudi Abdulahi na wanaume ni Nuhu Khamis na Yahya Omar.
Wagombea hao, kesho Jumatatu Januari 20, 2015,watapigiwa kura na Baraza Kuu kuwapata washindi.