Dar es Salaam. Hatua ya mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, inatajwa kuwa turufu kwa chama hicho.
Hilo linatokana na kile kilichoelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa, mtendaji mkuu huyo wa CCM ameishi katika siasa tangu ujana wake na mzoefu wa nafasi za utendaji serikalini ndani na nje ya nchi.
Lakini, kwa upande mwingine wanazuoni wanauchambua uamuzi huo wa Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, huku mmoja akijiuliza, kwanini imekuwa mapema kufanyika hivyo.
Rais Samia ametangaza uteuzi wa Dk Nchimbi leo Jumapili, Januari 19, 2025 katika mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.
Amesema uamuzi wa kumteua Dk Nchimbi umekuja baada ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuwasilisha kwake ombi la kupumzika na tayari amekabidhi barua rasmi.
“Anasema yeye ana miaka 68, angependa kuishi zaidi, ikiwezekana agonge 90 huko, akasema mama yake amefika 80 na. nilimbishiabishia, wiki iliyopita akanikabidhi barua hii.
“Na barua sikumjibu. Nilipokwenda kuzungumza na kamati kuu tukakubaliana tumpumzishe,” amesema Rais Samia.
Pamoja na kupongeza utendaji wa Dk Mpango kama msaidizi wake katika kipindi cha urais wake, amesema alizungumza na marais wastaafu, Jakaya Kikwete, Ali Mohamed Shein na Aman Abeid Karume na ndipo wakakubaliana jina la Dk Nchimbi.
“Jina moja hilo ndilo nimelipeleka kamati kuu na wao wamelikubali, nalileta kwenu jina la kijana wenu, Dk Emmanuel Nchimbi,” amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wajumbe.
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco, Dk Lazaro Swai amesema uteuzi wa mgombea mwenza huyo umezingatia utamaduni wa nchi.
Utamaduni huo, amesema ni wa kuhakikisha kama mgombea urais anatoka Zanzibar basi mgombea mwenza wake, muhimu atoke upande wa bara.
Hata hivyo, amesema ni mgombea mwenza sahihi kwa uzoefu wake katika siasa za Tanzania, kwa kuwa amekulia ndani ya CCM na siasa kwa ujumla wake.
Mbali na ndani ya chama, alieleza Dk Nchimbi amehudumu kwenye nafasi mbalimbali za Serikali ndani na nje ya nchi, anastahili kuwa mgombea mwenza.
“Hata akiwa Makamu wa Rais haitampa shida, kwa sababu ameshawahi kuduhumu kwenye nafasi za kiutendaji, hatashindwa kuwa msaidizi,” ameeleza.
Kwa upande wa mwanazuoni wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo ameutazama uamuzi huo wa Rais Samia kwa kujiuliza kwanini imekuwa mapema kiasi hicho.
Maswali zaidi, amehoji ilichukua muda kwa CCM kumchagua Makamu Mwenyekiti wake bara, imeshinikizwa na nini kumteua makamu na kumaliza la mgombea mwenza.
Swali lingine kwa mujibu wa Dk Masabo, uteuzi wa mgombea mwenza haikuwa moja ya ajenda iliyoorodheshwa mapema na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.
“Ni vema kujiuliza haya yaliyofanywa na CCM ni kwanini. Pia tujiulize kwanini mapema na je, uamuzi huo umefuata kanuni zao,” amesema.
Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, uamuzi wa mapema wa uteuzi wa mgombea mwenza huyo umelenga kukiepushia chama hicho migawanyiko, ambayo ingesababishwa na mbio za kuteuliwa.
“Lakini kufanya uamuzi huo sasa, kunaweza kukipunguzia migawanyiko. Mimi naona ni mbinu ya kukiepusha chama kuingia katika migawanyiko ya teuzi za wagombea,” amesisitiza.
Dk Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.
Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.
Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa. Alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.
Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.
Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika kilichokuwa Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).
Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.
Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya benki na fedha.
Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003–2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Dk Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.
Dk Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu.
Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.
Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.
Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.
Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013 kwa shinikizo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli juu ya “Oparesheni Tokomeza”.
Wakati watu wengi wanadhani Nchimbi aling’olewa uwaziri kwa shinikizo la Bunge, ukweli ni kuwa aliondoka kwa shinikizo la vikao vya CCM.
Ripoti ya kamati ya Lembeli ilieleza wazi kuwa anayepaswa kuwajibishwa ni waziri mmoja tu (Dk Mathayo David, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) lakini “party caucas” ya CCM ikawaangushia mzigo wengine watatu akiwamo Dk Nchimbi.
Lembeli aliwahi kukaririwa akisema: “Ripoti ilimtaja Dk Mathayo na sababu tulitoa mle ndani. Hao wengine watatu si kamati, ni mambo ya hukohuko kwenye party caucas. Ndiyo maana mara ya mwisho nilikwenda pale nikasema kuwa (Khamis) Kagasheki (Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, anaonewa.”
Machi mwaka 2017, akiwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dk Nchimbi aliwahi kukumbwa na msukosuko ndani ya chama chake, akapewa onyo kali na adhabu ya kutogombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minne.
Adhabu hiyo ilitokana na kilichoelezwa na CCM kuwa, ni usaliti katika uchaguzi wa mwaka 2015. Hata hivyo, makada wengine wa chama hicho walifutwa uanachama akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba.
Katika uchaguzi huo, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kumpendekeza Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.
Dk Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba walikuwa wanamuunga mkono Edward Lowassa aliyekuwa akiwania urais mwaka 2015 kupitia CCM kabla ya jina lake kukatwa na kutimkia Chadema.
Hata hivyo, baada ya mgombea urais kupatikana, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani na kueleza kwamba kama chama kimefanya uamuzi, mtu akiendelea kuupinga, huo ni usaliti.