Tutaanza na kisa tulichoshuhudia kwa ndugu yetu mmoja. Huyu bwana kuna kipindi aliachishwa kazi. Hivyo, alianza kuamka kila asubuhi akielekea mjini kusaka vibarua ili mkono uende kinywani.
Ulipita muda bila kuwa na namna ya kujiingizia kipato. Alifanikiwa kumtafutia mkewe kibarua kwa ndugu yake. Mama alifurahi kupata kibarua na kuingiza lau kipato. Hata hivyo, yule mama alianza kumuona mumewe kama hamnazo na asiye na ujanja wa kuhangaika na kupata kipato.
Siku moja, alidamka, kama kawaida yake akijiandaa kwenda kwenye kituo cha daladala kuelekea zake mjini kuchakarika. Kwa bahati mbaya, siku ile hakuwa hata na nauli. Hivyo, alimuomba mkewe nauli.
Badala ya mama kumpa nauli, alimjibu “mwanamume mzima unaomba nauli kwa mkeo! Mwanamume gani suruali.” Kwa busara na upendo, yule bwana hakukasirika wala kujibu zaidi ya kuumia ndani na kufunika kombe mwanaharamu apite.
Kwa vile tabia ile ilituudhi, tulimwita jamaa kando na kumpa nauli bila hata kumpa pole kwa kuhofia kuamsha uchungu hata kumwaga mafuta kwenye moto. Pamoja na kumhifadhi ndugu yetu huyu, kile kitendo kilituudhi na kutufedhehesha.
Katika hali hii, mume akipata fursa ya kutosha, je, hawezi kulipiza kisasi kiasi cha kuanza unyanyasaji katika ndoa? Je, hapa chanzo na wa kumlaumu zaidi ya mkewe ni nani japo naye, kama mume, anapaswa kupima mambo?
Je, ni wangapi wanatumia lugha chafu kama hizi dhidi ya wenzi wao? Je, wanafaidikaje au kuathirikaje na tabia hii chafu? Kwa ufupi, haukupita muda, wanandoa hawa waliachana. Hapa kuna mambo kadhaa ya kujifunza.
Mosi, kupata na kukosa, ni majaliwa. Aliye nacho leo anaweza asiwe nacho na asiye nacho akawa nacho kesho.
Pili, kuna haja ya kuvumiliana, hasa wanandoa wanapopata mitihani ya kimaisha ambayo ni mambo ya kawaida yanayoweza kuwajenga au kuwabomoa.
Tatu, kupata si ujanja na kukosa siyo uzembe au ujinga. Kwa nini watu wa namna hii hawahoji ni kwa nini watu wengine wanaishi kwa muda mrefu wakati wengine wanaishi kwa muda mfupi?
Nne, upendo baina ya wanandoa unapaswa kuvuka vitu vidogo kama vile kipato, elimu, na mengine kama haya. Kwani, kila mmoja anaweza kuwa nayo au asiwe nayo.
Tuliwahi kudurusu kisa cha mwanandoa mmoja aliyesoma akaishia form four failure aliyejiona msomi sana kuliko mumewe ambaye hakumaliza hata la saba. Huyu mama kutoka familia maskini, alianzishiwa biashara na mumewe huyo huyo asiyesoma na kufikia hata kumilki biashara yake na gari.
Baada ya kujiona kapata, alianza kumdharau mumewe hadi kufikia kumtamkia “wewe hukusoma.” Ajabu ya maajabu, wakati wanakubaliana kuoana, alijua fika kuwa mumewe alikuwa kaishia darasa na tano. Kwa waliosikia kisa hiki cha hovyo, walijiuliza ni kwa nini hakumkataa alipomchumbia kutokana na kutokuwa na elimu aliyotaka ijapokuwa naye hakuwa nayo? Kama kisa cha kwanza, ndoa ilivunjika.
Ukiunganisha kisa cha ‘mume suruali’ na cha ‘wewe hukusoma’ unagundua mambo mengi ambayo ni hatarishi na sumu katika ndoa. Mfano, mwanandoa aliyemwambia mwenzie ni mume suruali, naye alikuwa katokea kwenye familia maskini. Je, kwa nini hakujiuliza kuwa hata baba yake alikuwa mume suruali na mama yake mke gauni? Epuka kumhukumu mwenzio kabla ya kujihukumu.
Kama mmejaliwa au mmoja wenu kajaliwa talanta fulani, zitumieni kwa upendo na usawa bila kudhalilishana, kunyanyasana, kutukanana, na kuvunjiana heshima.
Leo unaweza kumuona mwenzio hafai wakati nawe hufai na kesho mkaachana ukajikuta umemkimbia mjusi na kumkumbatia mamba. Hivyo, kabla ya kuhukumu au kutuhumu, fanya hivyo kwako mwenyewe kwanza. Hiyo ndiyo busara ya leo.