Get Program inayoshiriki Ligi ya Wanawake (WPL) imempa mkataba wa mwaka mmoja aliyewahi kuwa kocha wa Ceasiaa Queens, Miraji Fundi.
Fundi alikuwa miongoni mwa makocha watatu waliopita Ceasiaa kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi akiwemo Petro Mrope na Shabani Said kabla ya Ezekiel Chobanka kupewa kandarasi ya kuiongoza timu hiyo.
Chanzo kutoka Get Program kililiambia Mwanaspoti viongozi wamempa mkataba wa mwaka mmoja kocha huyo wa zamani wa Ceasiaa.
Tangu msimu uanze Get Program iliyopanda daraja kutoka Ligi ya Mkoa haikuwa na kocha maalum.
“Tulianza msimu bila ya kuwa na kocha maalum kutokana na changamoto mbalimbali za kifedha hatukuanza Pre Season vizuri kwa hiyo angalau sasa yamekaa sawa, ndiyo tumeanza usajili,” kilisema chanzo hicho.
Kiliongeza, pia timu hiyo imeongeza wachezaji wapya baada ya nyota watano kutimka kikosini hapo.
Kocha huyo msimu uliopita alikuwa na Baobab Queens iliyoshuka daraja.