Unguja. Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), ikitangaza bei mpya elekezi kwa watumiaji wote wa umeme Zanzibar, imetaja sababu ya mabadiliko hayo ni kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya umeme Visiwani Zanzibar.
Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni miaka tisa tangu yafanyike mabadiliko ya mwisho mwaka 2016 na bei hizi mpya zitaanza kutumika Januari 20, 2025 kwa makundi yote manne ya utumiaji nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Zura, ilipokea maombi ya kubadilisha bei za umeme kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya umeme Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Zura jana jioni, bei hizo zimetoa punguzo la Sh190 kwa watumiaji wadogo ambao walikuwa wakilipa Sh480 kwa uniti kila wanapovuka matumizi ya uniti 50 kwa mwezi, ambapo kwa sasa watalipa Sh290 badala ya Sh480 wakivuka uniti hizo.
Hata hivyo, katika kundi hili ambalo ndio la watu wa chini kabisa kwenye matumizi, gharama ya kununua uniti moja imeongezeka kutoka Sh79 hadi Sh84 sawa na ongezeko la Sh5.
Meneja kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Haji amesema tozo ya kutoza huduma kwa watumiaji hawa wadogo kuanzia uniti 0 hadi 50 itaendelea kuwa Sh2,100.
Wateja wenye matumizi ya kawaida, uniti moja hadi 1,500 bei ya kununua uniti moja imepanda kutoka Sh266 hadi Sh280 huku kila uniti inayoongezeka ikitoka Sh288 hadi Sh310 na tozo ya kutoa huduma itaendelea kuwa Sh2,100.
“Hawa ni wateja wenye matumizi ya kawaida hususani majumbani wenye biashara ndogondogo, maduka, mabango, waliounganishwa katika msongo mdogo wa umeme kwenye njia moja (230V) na njia tatu (400V),” amesema.
Kwa wateja waliounganishwa katika msongo mdogo na msongo wa kati wa umeme, bei ya uniti moja imeongezeka kutoka Sh206 hadi Sh217 huku bei ya mahitaji ya juu (kila uniti inayoongezeka) itabaki ile ya wali Sh16,000 na tozo ya kutoa huduma itaendelea kuwa bei ileile ya Sh10,500.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, wateja waliounganishwa katika msongo mkubwa wa umeme bei ya uniti moja itakuwa Sh178 kutoka Sh169, bei ya mahitaji ya juu itaendelea kuwa Sh16,000 na bei ya tozo itaendelea kuwa ilile ya Sh150,000.
Mbaraka amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanya tathmini ya kina ikiwemo kukutana na wadau ili kupata maoni yao.
Wakati bei zikibadilika, baadhi ya wananchi wameonekana kutokuwa na ufahamu, huku wakiomba kupewa elimu zaidi kuhusu mifumo hiyo.
“Hapa watu wengi watakuwa wanalipia gharama kubwa bila kujua na ndio maana kuna wakati mtu ananunua umeme anaona kidogo. Nasema hivi kwa sababu watu hawaelezwi kama kuna kiwango wanalipia ikiwa zitaongezeka uniti kwa mwezi,” amesema Haji Mbarok, mkazi wa Magogoni.
Mwananchi mwingine, Rahma Abdul amesema licha ya kupunguza kiwango cha uniti zinazozidi, bado mamlaka isingeongeza kiwango cha uniti katika matumizi ya kawaida.