Maniche awatoa hofu Mtibwa Sugar

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’ amesema licha ya timu hiyo kutosajili mchezaji yeyote dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mashabiki wasiwe na hofu kwa sababu wachezaji wao muhimu wote wamewabakisha.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maniche alisema benchi la ufundi hawana hofu na kutofanyika kwa usajili kwa sababu tayari wachezaji wao wote muhimu hakuna aliyeondoka, hivyo mashabiki watarajie makubwa kutokana na upana wa timu hiyo.

“Tangu mwanzoni tulijitahidi kuhakikisha kila nafasi inakuwa na wachezaji zaidi ya wawili hadi watatu wenye viwango sawa ambao watatusaidia kufanikisha malengo yetu, jambo nzuri pia dirisha hili wengi wao muhimu tumewabakisha hapa kikosini.”

Kocha huyo anayekiongoza kikosi hicho baada ya kuondoka Mmarekani Melis Medo aliyejiunga na Kagera Sugar, alisema presha ni kubwa ya kuipambania timu hiyo irejee tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, ila watapambana licha ya ushindani uliokuwepo.

Timu hiyo kwa sasa inaongoza Ligi ya Championship ikiwa na pointi zake 38, baada ya kucheza michezo 15, ikishinda 12, sare miwili na kupoteza mmoja tu, imefunga jumla ya mabao 26, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Related Posts