Dar es Salaam. Mtandao wa TikTok umeacha kufanya kazi nchini Marekani, saa chache kabla ya sheria mpya inayopiga marufuku mtandao huo kuanza kutekelezwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), mtandao huo umepigwa marufuku kutokana na wasiwasi kuhusu uhusiano wake na Serikali ya China na ilipewa tarehe ya mwisho ya Januari 19, 2025.
Rais Joe Biden amesema kuwa ataliacha suala hilo kwa mrithi wake, Donald Trump ambaye naye pia amesema kuwa huenda atatoa msamaha wa siku 90 kwa TikTok atakapoingia madarakani kesho Jumatatu.
“Kuongezwa siku 90 ni jambo ambalo huenda likafanyika, kwa sababu ni sahihi. Ikiwa nitaamua kufanya hivyo, labda nitatangaza Jumatatu,” Trump aliambia NBC News jana Jumamosi.
Hata hivyo watumiaji waliripoti kuwa programu hiyo pia imeondolewa kwenye programu za Apple na Google za Marekani hivyo TikTok.com haikuonyesha video.
Mahakama Kuu ya nchini humo juzi Ijumaa ilithibitisha sheria hiyo, iliyopitishwa Aprili mwaka jana, inayopiga marufuku programu hiyo nchini Marekani isipokuwa kampuni mama yake iliyoko China, ByteDance, iuze jukwaa hilo kufikia Jumapili, jambo ambalo haijafanya.
TikTok imesema kuwa sheria hiyo inakiuka ulinzi wa uhuru wa kujieleza kwa watumiaji wake milioni 170 nchini humo.
Baada ya uamuzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TikTok, Shou Zi Chew amemuomba Rais mteule Trump na akimshukuru kwa nia yake ya kufanya kazi nao na kutafuta suluhisho. Aidha Chew anatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa Trump kesho Jumatatu.