Mastraika Mbeya wamkosha Massawe | Mwanaspoti

KATIKA kuhakikisha Mbeya Kwanza inafanya vizuri ili kutimiza malengo ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, kocha wa timu hiyo, Emmanuel Massawe ameweka wazi kuridhishwa na safu yake ya ushambuliaji hadi sasa, tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.

Massawe alisema hadi sasa safu ya ushambuliaji imeonyesha matumaini makubwa tofauti na walivyoanza msimu na licha tu ya changamoto za eneo la kujilinda ila angalau kuna mwanga mzuri uliopo mbeleni, hivyo kilichobakia ni mapungufu madogo.

“Kwa sasa kumekuwa na muunganiko mzuri kuanzia safu ya kiungo na ushambuliaji kitu ambacho kimetengeneza balansi nzuri katika timu, changamoto zilizopo ni ndogo ambazo tunazifanyia kazi siku baada ya siku ili tuwe bora zaidi ya sasa hivi.”

Akizungumzia usajili wa mshambuliaji, Ditram Nchimbi aliyetokea Biashara United huku akiwahi kuzichezea Yanga na Mbeya City, Massawe alisema mchezaji huyo ameonyesha matumaini makubwa jambo linalomfanya kujivunia usajili wake kikosini humo.

Masawe anapigania timu hiyo irejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2021-2022 na katika michezo yake 15 imeshinda minane, sare mitatu na kupoteza minne, ikifunga mabao 18 na kuruhusu 14, ikishika nafasi ya sita na pointi 27.

Related Posts