MUFTI MKUU TANZANIA KUJA NA ZIARA YA KUIMARISHA UONGOZI MKOA WA DODOMA

 


Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zubeir amesema Baraza limepanga kufanya ziara rasmi mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kutembelea mikoa yote 26 nchini. Ziara hii inalenga kuimarisha uongozi, kushughulikia changamoto, na kuweka mipango madhubuti kwa maendeleo ya kidini na kijamii. Katika ziara hiyo, viongozi wa Baraza watazunguka kila wilaya kujadili mafanikio na changamoto zilizopo, huku wakishirikiana na viongozi wa ngazi za kata, wilaya, na mkoa katika kupanga mikakati ya utekelezaji.

Aidha amesema Lengo kuu la ziara hii ni maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wa Baraza. Masuala ya uchaguzi yatapewa uzito mkubwa, ambapo viongozi wamehimizwa kuwa makini katika kuchagua watu wenye uwezo na maadili bora. Kukosea katika uchaguzi wa viongozi kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi wa Baraza na maendeleo ya Uislamu.

Baada ya ziara kukamilika katika mikoa yote, Baraza litafanya mkutano mkuu kwa lengo la kupitisha rasmi viongozi waliochaguliwa ili waanze kutumikia jamii katika maeneo yao. Masheikh, Wenyeviti, Makatibu, na viongozi wengine wa ngazi zote wamekumbushwa umuhimu wa jukumu lao katika kuhakikisha wanachagua viongozi wenye dhamira ya dhati ya kulinda na kuimarisha Uislamu.

Ziara ya Dodoma, pamoja na mikoa mingine, ni hatua muhimu katika kufanikisha malengo ya Baraza, ikiwa ni maandalizi ya kuweka uongozi imara unaoendana na mahitaji ya jamii. Viongozi wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu kwa kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa uaminifu na uadilifu.

Related Posts