BAADA ya KMC kukamilisha usajili wa mshambuliaji, Shaaban Idd Chilunda, kocha wa kikosi hicho Kally Ongala amesema nyota huyo atawashangaza wengi kutokana na uzoefu aliokuwa nao, huku akiweka wazi ni mojawapo ya mapendekezo yake kikosini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ongala alisema moja ya mapendekezo yake yalikuwa ni kuongezewa nguvu eneo la ushambuliaji na kitendo cha kumpata mshambuliaji huyo, anaamini kitaongeza chachu kwa kushirikiana na nyota wengine wapya na waliopo.
“Tumefanya usajili kutokana na mahitaji ya timu, nashukuru tumepata wachezaji wazoefu ambao sasa naamini katika raundi ya pili wataleta mabadiliko chanya kuanzia uchezaji na mbinu mbalimbali ambazo zitatusaidia kusogea nafasi tano za juu.”
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema usajili wa nyota huyo ni moja ya mapendekezo ya benchi la ufundi, huku akiweka wazi hawajafanya maboresho makubwa kwa sababu waliopo wengi wao hawakuondoka kikosini.
Chilunda aliwahi kuichezea timu hiyo kwa mkopo Januari mwaka jana akitokea Simba ingawa aliachana nayo Julai mwaka jana, huku akizichezea Azam FC, CD Tenerife ya Hispania na Moghreb Atletico Tetouan ya Morocco na sasa amerejea mara ya pili.
Akiwa na Simba Chilunda hakufunga bao lolote la Ligi Kuu Bara ingawa wakati akiichezea KMC alifunga moja katika mchezo ambao kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni kilitoka sare ya 1-1, dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania Februari 27, 2024.
Ongala alihitaji kuboresho eneo la ushambuliaji ili kuongeza nguvu na nyota waliopo ambao ni Daruweshi Saliboko ambaye hadi sasa amefunga mabao mawili tu, huku timu hiyo ikifunga 11 na kuruhusu 21, katika michezo 16.