Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma
WAZIRI Mkuu mstaafu Mizengo Pinda pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Abdulrahman Kinana wamemzungumzia Stephen Wasira ambaye amepitishwa na Chama hicho kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupigiwa kura ya ndiyo 1910 na wajumbe wa mkutano mkuu maalum.
Akimzungumzia Wasira,Waziri Mkuu Mstaafu Pinda amesema ni kiongozi mwenye uzoefu wa kutosha katika njanja za kisiasa hivyo atakisaidia Chama hicho kuendelea kushika dola.
Pinda amesema kuwa anamjua Wassira kama kada mahiri katika Chama hicho na aliposoma historia yake ilimshutua kumbe sio kama alivyokuwa anamfikiria kwani aliibuka tangu enzi za TANU mwaka 1959.
Ameongeza kwamba Wasira alipata kadi ya uanachama akiwa na miaka 16 na amekuwa kwenye nafasi mbalimbali na kote huko ameonesha uwezo mkubwa kichama na shughuli za serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake Abdulrahman Kinana amempongeza Wassira kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara na kwamba amewahi kufanya naye kazi hivyo anajua umahiri na uadilifu wake,hivyo anaamini anakwenda kukisaidia Chama.
Akisoma Azimio la Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kuhusu wasifu wa Wassira, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mohammed Said Dimwa, amesema Wassira ni muumini wa kweli wa siasa za chama chao cha ujamaa na kujitegemea.
Pia anazingatia kikamilifu masharti ya wanachama, sifa na miiko ya kiongozi kama ilivyoainishwa katika Katiba ya CCM na daima amekuwa mstari wa mbele kupigania na kulinda maslahi ya chama hicho.
“Wassira ni mkweli, mnyenyekevu, anapenda nchi yake, raia mwema wa Tanzania, muumini wa muungano katika serikali mbili, mwanamapinduzi anayependa maendeleo ya nchi na kuchukia rushwa kwa vitendo.”