KUNANI Tanzania Prisons? Licha ya kuletwa kocha mpya, Aman Josiah habari ya kushtua ni kuona wakongwe wa timu hiyo wakiondolewa.
Habari ambazo Mwanaspoti limepenyezewa ni uongozi wa juu katika Jeshi la Magereza (Kitengo cha Michezo) limewachomoa manahodha wao, beki wa kulia Salim Kimenya na kiraka Jumanne Elfadhili kuendelea kuitumikia timu hiyo na kuhamishiwa katika majukumu mengine.
Mwanaspoti linafahamu, manahodha hao ambao kitaaluma ni askari Magereza, Kimenya na Elfadhili walipewa barua za kuhamishwa kimajukumu tangu juzi licha ya kocha Josiah kutokukubaliana na jambo hilo.
Chanzo kutoka ndani ya Prisons, kililidokeza Mwanaspoti, benchi la ufundi lilitaka kuendelea na huduma ya wachezaji hao waandamizi wa timu kwani mchango wao ulihitajika lakini viongozi wa juu ndio walisisitiza warejeshwe kwenye majukumu yao mengine nje ya timu.
“Sijajua ni wachezaji wakongwe wote wanaondolewa au vipi, kwa sababu Kimenya na Elfadhili wamepelekwa vikosi tofauti kabisa kuendelea na majukumu yao, mmoja Iringa na mwingine hapa hapa Mbeya,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Licha ya kina Kimenya kuondoka bado wachezaji wengine kama Mbangula (Samson) na Jeremiah (Juma) wao pia ni kama vile wamekalia kuti kavu na wanaweza wasionekane kabisa kweye Ligi Kuu mzunguko huu kama ilivyo kwa wenzao.”
Alipotafutwa Elfadhili juu ya kuondoka kwake simu yake haikupatikana, lakini kwa upande wa Kimenya alipotafutwa alijibu ni kweli lakini jambo hilo hawezi kulizungumzia kwa sasa.
“Ni kweli sitokuwepo kwenye duru la pili na timu, lakini siwezi kuzungumzia kiundani, ikifika muda wake nitazungumza,” alisema.
Mwanaspoti halikuishia hapo lilimtafuta kocha Josiah aliyekiri kupokea taarifa hizo, lakini itambidi akune kichwa na kutumia rasilimali nyingine alizonazo.
“Kimenya na Elfadhili ni wachezaji wazuri hakuna asiyejua hilo na nilitamani kufanya kazi nao, siyo kwamba viwango vimeshuka ila kilichotokea ni utaratibu wa kazi kutoka kwenye mamlaka,” alisema kocha huyo wa zamani wa Geita Gold na Biashara United.
Akizungumzia kuhusu pengo la manahodha hao waliokuwa wanaunda kikosi cha kwanza, alisema kwa sasa ni ngumu moja kwa moja kukiri mapengo yao kwani bado hawajacheza mechi yoyote.
“Bado sijacheza mechi ya ushindani, ninachofanya sasa ni kutengeneza wachezaji wangu nilionao kuziba nafasi za waliiondoka; “Tukicheza ndio tutaona na nyie mtaona kama kuna pengo waliopo na kuitetea timu.”
Kimenya na Elfadhili walianza kuitumikia timu ya Prisons msimu wa 2013/14 hadi sasa.