Dodoma/Dar. Kama kuna mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye ndoto ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, basi asahau, kwani wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho wamefunga milango.
Kwa kauli moja, wajumbe wameazimia Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atakuwa mgombea urais wa chama hicho wa Tanzania, huku Zanzibar atakuwa, Dk Hussein Ali Mwinyi atapeperusha bendera ya CCM.
Mkutano mkuu huo maalumu ulioanza jana Jumamosi na kumalizika leo Jumapili, Januari 19, 2025 jijini Dodoma, pamoja na mambo mengine, ulikuwa na ajenda tatu tu: kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti-Bara kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana, kupitisha mabadiliko ya Katiba ya CCM, pamoja na kusomwa kwa utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kuanzia Novemba 2020 hadi Desemba 2024.
Ajenda ya kwanza ya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti ikafanyika, na kada mkongwe Stephen Wasira akachaguliwa kwa kura 1,910 (asilimia 99.42), huku kura saba zikimkataa. Uchaguzi huo ulifanyika jana Jumamosi.
Leo Jumapili, mkutano mkuu maalumu umeketi kukamilisha ajenda ya kusomwa taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, inayoongozwa na Dk Mwinyi, pamoja na Tanzania Bara, chini ya Rais Samia. Katika taarifa hizo, Makamu wa Kwanza wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, akisoma kwa upande wa Zanzibar, na Kassim Majaliwa akisoma ya Tanzania Bara.
Baada ya kusomwa kwa taarifa hizo, wajumbe walipata nafasi ya kuchangia, na hapo akaibuka Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza, Mwasi Kamani, aliyebadili upepo na ratiba nzima ya mkutano huo kwa kutoa hoja ya kutaka wajumbe kutamka kwa kauli moja kuwa Rais Samia na Dk Mwinyi wathibitishwe kuwa wagombea urais wa CCM.
Uamuzi wa mkutano mkuu huo kuwapitisha Samia na Dk Mwinyi kunafunga milango kwa wanachama wengine wa chama hicho waliokuwa wakitamani kujitosa kuomba ridhaa ndani ya chama hicho.
Hiyo inamaanisha Rais Samia ataingia kwa mara ya kwanza kuwaomba ridhaa ya wananchi kumchagua kuwatumikia, akichuana na wagombea wa vyama vingine akiwemo wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, ambaye ameweka nia kupambana na Samia wakati ukifika.
Samia aliyekuwa Makamu wa Rais aliingia Ikulu Machi 19, 2021 baada ya Rais John Magufuli kufariki dunia (Machi 17, 2021), hivyo kwa mujibu wa Katiba aliapishwa kumalizia kipindi kilichoanzwa na Magufuli.
Upande wa Zanzibar safari hii, Dk Mwinyi anatarajia kuchuana na wagombea wengine, akiwemo wa ACT-Wazalendo, Othuman Masoud, ambaye ameshaweka nia na kuzindua timu ya ushindi. Othuman ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa visiwa hivyo.
Vyama vingine vya siasa, ukiacha ACT-Wazalendo, bado havijatangaza utaratibu wa kupata wagombea wa nafasi ya urais.
Kamani alivyobadili upepo
Baada ya Majaliwa na Abdulla kuwasilisha taarifa zao, uliwadia wasaa wa wajumbe kuzijadili, na miongoni mwao waliozijadili ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mwasi Kamani.
Kamani amesema kitendo cha makundi mbalimbali, ikiwemo bodaboda, watoto wa shule, wazee, na machinga kumchangia Rais Samia fedha ili achukue fomu ya kugombea kinaonyesha utendaji bora, hivyo hakuna budi aendelee kuongoza Tanzania.
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji, amesema utekelezaji wa ilani hiyo umefanyika kwa asilimia 100 na umefikia kipindi kama wajumbe hawana deni na mwenyekiti wa chama hicho cha CCM.
“Hata kama mtu haoni, akipapasa anajua hapa kazi imefanyika. Tumeona hospitali za wilaya, mikoa, meli na barabara zikijengwa kila kona, umepunguza vifo vya wajawazito,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, amesema miradi iliyotekelezwa imewagusa watu wote si Tanzania Bara pekee bali hadi visiwani Zanzibar.
“Kutokana na utekelezaji huo, mkutano mkuu unatoa azimio Rais Samia agombee nafasi hiyo pia, Dk Mwinyi awe mgombea wa urais Zanzibar,” amesema Kimbisa.
Baada ya maelezo ya wajumbe hao ambao walipokuwa wakichangia walikatizwa na shangwe za wajumbe wakiwaunga mkono.
Wakati wajumbe hao wakichangia, hususan Kamani, Rais Samia alikuwa akiteta jambo na Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete. Baada ya hapo, Rais Samia akampa fursa Kikwete kwa niaba ya wastaafu kusema jambo juu ya hoja hiyo.
Kikwete amesema kila chama kina utaratibu wake wa kuteua wagombea, na uamuzi ni wa kikao hicho, na kwamba kuna nchi kama Namibia wanafanya uamuzi wa wagombea mwaka mzima.
“Kama tunataka kuamua leo Samia na Mwinyi ni wagombea wetu, mamlaka hayo tunayo. Kama tunaamua hivyo, ndiyo tumeamua. Kilichobaki ni ushauri wa wale wanaojua taratibu za sheria, lakini watu wote watajua tu kuwa CCM kwenye uteuzi wa wagombea imemaliza,” amesema.
Amesema kazi kubwa imefanywa na viongozi hao kupitia taarifa ya utekelezaji wa ilani iliyowasilishwa kwenye mkutano huo, imeonyesha wana-CCM hawakukosea kwa kuwa ni watu makini, wanajua wanachofanya na kinachotakiwa kufanyika.
“Ushindi wa CCM ni dhahiri, ushindi kwa mwaka huu hauna mjadala. Wagombea watakuwepo wa vyama vingine, lakini sioni namna wanavyoweza kuishinda CCM. Lakini sio kwa ujanja ujanja, yapo mambo mengi mazuri yaliyofanywa na Serikali zetu na yana manufaa kwa Watanzania, kwa sababu mnaweza kufanya mambo mengi mazuri lakini hayajawagusa Watanzania. Haya yanagusa maisha,” amesema.
Amesema wananchi watatambua na kuthamini kazi iliyofanywa na viongozi hao na kushauri wana-CCM wasibweteke.
“Siku zote jipe rai kwamba uchaguzi huu utakuwa mgumu. Hiyo ndiyo falsafa ya jeshi, maandalizi yetu yawe kwamba tunakwenda kwenye vita kubwa na si ndogo, na tujiandae kwamba tunakwenda kwenye mapambano makubwa. Lazima tujiandae vizuri, na mimi niliyoyasikia hapa, bwana aah! Sijui labda kutokee mchawi, na wachawi walishakufa, hawapo tena,” amesema.
Kikwete amesema wajumbe wa mkutano wanamtaka Samia na Mwinyi waendelee na kwamba hakuna wa kusema Hapana. Kauli hiyo imeibua shangwe ukumbi mzima wakiimba, “CCM… CCM… CCM… CCM.”
“Namna ya kulifanya jambo hili liandaliwe azimio maalumu la mkutano ili kutamka, liletwe, na ithibitishwe na linakubaliwa na inakuwa sasa rasmi uamuzi wa mkutano mkuu,” amesema.
Amewaomba viongozi na wajumbe kuwaeleza wanachama yaliyofanyika chini ya uongozi wao na sababu ya kuwapitisha kuwapa ridhaa tena.
Alimpongeza Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi, kwa utendaji wake mzuri huku akieleza kuwa Makamu Mwenyekiti-Bara, Stephen Wasira, uwezo wake wa uongozi, kupambana, na kujenga hoja unajulikana, na nafasi hiyo imepata mtu madhubuti.
Amesema mkutano huo umemuonyesha sura ya CCM anayoijua, kwa kuwa mikutano mikuu ndiyo inaonyesha nguvu ya kuendelea mbele, na hana shaka wajumbe watarudi na nguvu mpya.
Azimio liliandaliwa na sekretarieti, na ilipomalizika, likasomwa na mtoa hoja, Kamani, mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu. Amesema kwa kuzingatia mamlaka waliyonayo kwenye Katiba ya CCM chini ya Ibara ya 101, kifungu kidogo cha 5b, wameazimia jina hilo kuwa ndiyo mwanachama atakayesimama kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Azimio la Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa uliofanyika Dodoma kuhusu kuteuliwa kwa wagombea wa urais Tanzania Bara na Zanzibar Januari 19, 2025, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa tuliokutana kwa pamoja katika kikao maalumu tukiwa 1924, kwa pamoja tumeazimia Samia Suluhu Hassan agombee Urais.
“Hivyo, tunaiagiza Halmashauri Kuu ya CCM Taifa nayo kwa upande wake kutekeleza jukumu lake hilo leo Januari 19, 2025,” amesema.
“Pia, katika azimio la pili, kwa kuwa chini ya Ibara ya 103(c) Katiba ya CCM mwaka 1977 toleo la Desemba 2022, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ndicho kikao chenye madaraka ya kumchagua mwanachama atakayegombea Zanzibar, tunaelekeza kikao kukutana leo kutekeleza kikao kitakachomchagua Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kugombea Urais,” amesema Kamani.
Baada ya kuwasilisha, mwenyekiti wa mkutano huyo aliwahoji wanaounga na wote walikubali huku akiahirisha mkutano huo kwa muda ili Halmashauri Kuu ikutane kutekeleza takwa hilo la azimio.
Mchambuzi wa siasa, Dk Paul Loisulie amesema si jambo la kushangaza kwa CCM, kwani imekuwa ni utaratibu wake kwa mtu aliye kwenye kiti akigombea kwa mara ya pili kumuacha agombee.
Amesema CCM wanachofanya ni kuziba mianya ya mwanachama mwingine anayetaka kugombea ili wawekeze nguvu katika kushindanisha na wagombea wa nje ya chama.
“Faida yake ni kwamba inaondoa makundi na kuepusha ushindani wa wagombea ndani ya chama, bali nguvu iwekezwe nje ya chama. Ukiruhusu ushindani kwa Rais aliyepo madarakani ndani ya chama, unaweza kuibuka makundi na kugawanya chama,” amesema.
Amesema kitendo cha kuepuka makundi ni maamuzi ya ndani ya chama kwamba aliyepo amalizie, na ina faida, inaondoa ushindani wa makundi pale ambapo kila mmoja akiwa huru.
“Akijitokeza mwingine, maana yake anampinga mwenyekiti wake, na itabidi atafute maeneo ambayo mwenyekiti wake hakufanya vizuri ili alete ushindani,” amesema Dk Loisulie.
Kwa upande wake, Dk Frank Mateng’e kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema CCM siku zote wanakwenda na jina la Rais aliyepo madarakani na ni utamaduni kwa miaka yote.
“Utamaduni huu umefikia hatua ikitokea mtu anasema anataka kugombea na mwenyekiti aliyepo madarakani, kwanza chama kinahamaki juu yake, na ilishawahi kutokea huko nyuma.
“Faida yake ni utulivu ndani ya chama, na yule mwenyekiti anaweza kufanya mambo yakaenda, badala ya kuanza makundi na kuanza kampeni ndani ya chama. Changamoto yake inakuja kwa wale wanaotaka kujaribu nafasi hiyo, wanakuwa hawana nafasi,” amesema.
‘Uamuzi wa Kihistoria’
Makada wa CCM wameeleza kuwa tukio hili ni la kwanza katika historia ya chama hicho kwa miaka ya hivi karibuni, kutolewa hoja kisha kutangazwa kwa azimio la kuwathibitisha wagombea wa nafasi ya urais mwanzoni mwa mwaka.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, wajumbe wa Mkutano Mkuu wanaweza kupendekeza kwa kuwasilisha hoja na kama itaungwa mkono na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), basi azimio hilo litakuwa limepitishwa na itakuwa marufuku kwa mwanachama mwingine kujitokeza kuitaka nafasi hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi baada ya azimio hilo kupitishwa, mjumbe wa mkutano huo kutoka Kagera, George Ruhoro, amesema kilichofanyika ni kufunga njia katika suala la wagombea urais kwa pande zote mbili ili mambo mengine muhimu ya kusaka ushindi kwenye uchaguzi mkuu, yasonge mbele.
“Leo tumemaliza kazi, sasa kama kuna mtu anaota kuja kugombea urais kwa tiketi ya CCM, basi hiyo imeenda. Shughuli ndiyo imeisha. Kama kuna mtu aliyekuwa na ndoto hizo, labda akagombee kwenye chama kingine,” amesema Ruhoro, ambaye pia ni Mbunge wa Ngara.
Amesema uamuzi huo umetokana na Watanzania kuguswa na utendaji kazi wa viongozi wa kitaifa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika, amesema wajumbe wameona hakuna haja ya kuweka sintofahamu ya kutofahamika kwa wagombea wa CCM hadi Bunge litakavyovunjwa.
Amesema wameamua kufanya hivyo ili wakitoka katika mkutano huo, waende kuwaeleza wananchi kuwa hakuna wagombea wengine wa CCM bali ni hao wawili kwenye nafasi hiyo.
“Sababu ni moja tu, ni yaliyofanyika hayajawahi kutokea hata kwangu Njombe na watu walio humu ndani ni mashahidi. Tumeona video za miradi ya maendeleo kwa dakika 40, kuna maeneo huwezi kufikiria kama uko Tanzania,” amesema.
Naye Profesa Adolf Mkenda, mbunge wa Rombo, amesema hata wasingefanya jambo hilo, hakuna mwanachama angejitokeza kuitaka nafasi hiyo zaidi ya Rais Samia na Dk Mwinyi kwa upande wa Zanzibar.
“Ni utamaduni wetu, watu wanaupenda kwa sababu ya utekelezaji mzuri wa Ilani… Lakini kila mtu angeweka mambo yote yaliyofanyika, pengine tungekuwa na kutwa nzima kujieleza,” amesema Profesa Mkenda.
Waziri huyo wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema uamuzi huo si jambo la ajabu na kuwataka watu kukumbuka walikotoka kwa kuangalia marais wengine waliokaa madarakani vipindi viwili.
Baada ya kikao kurejea, Rais Samia amesema kabla ya kuanza kwa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC), walitengua kanuni na kuruhusu Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar kukutana ijadili, kisha kutoa mapendekezo.
Baada ya hatua hiyo, Halmashauri Kuu ya Taifa ilijadili na kupiga kura 192 na moja iliharibika.
Rais Samia amesema kura mbili zilikuwa za hapana, na ndiyo 189, sawa na asilimia 98.43. Walipohojiwa wajumbe wa mkutano huo maalumu walikubali kwa kunyoosha mikono.
Baada ya matokeo hayo, Rais Mwinyi akasema: “Niwashukuru sana wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kuthibitisha uteuzi wangu. Asanteni sana.”
Dk Nchimbi Mgombea Mwenza
Katika mkutano huo, moja ya mambo mengine yaliyoibua shangwe na mshangao ni Rais Samia kupendekeza jina la Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi huo.
Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Januari 15, 2024, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichofanyika Unguja, visiwani Zanzibar. Alichukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo, aliyejiuzulu Novemba 29, 2023.
Rais Samia alimpendekeza Dk Nchimbi akisema ni baada ya makamu wake, Dk Philip Mpango, kuomba kupumzika. Amesema jina hilo lilipendekezwa baada ya kushauriana na marais watatu wastaafu—Jakaya Kikwete, Amani Abeid Karume, na Dk Ali Mohamed Shein.
“Lakini kama mnavyojua, Dk Philip Mpango ndiye Makamu wa Rais. Amekuja kuniomba nimpumzishe; ana sababu kadhaa, lakini sio za mahusiano ya kazi.
“Anasema yeye ana miaka 68, angependa kuishi zaidi—ikiwezekana afikishe miaka 90. Akasema mama yake amefika 80 na zaidi. Nilimbishia, lakini wiki iliyopita akanikabidhi barua hii. Barua sikumjibu. Nilipokwenda kuzungumza na Kamati Kuu tukakubaliana tumpumzishe.
“Lakini nataka niwaambie, mambo tuliyoyaona pale yanapita-pita ni kwa msaada wake. Nimemtuma sana. Kwa kweli, baada ya maelezo yake na baada ya kueleza katika Kamati Kuu, tumemshukuru sana kwa kazi aliyotufanyia na atakavyoendelea kufanya ndani ya mwaka mmoja. Lakini bado yupo,nitaendelea kumtumia.
“Sasa baada ya kupata barua ya Makamu wa Rais, tukahangaika kutafuta, tukaanza kufikiria nani anaweza kunisaidia, kunong’ona nao, kuangalia labda waliokuwa tunawafikiria, na wote tukakubaliana na jina moja.
“Jina moja hilo ndilo nimelipeleka Kamati Kuu, na wao wamelikubali. Sasa nalileta kwenu jina la kijana wenu, Dk Emmanuel Nchimbi,” amesema Rais Samia huku ukumbi ukilipuka kwa shangwe.