Rombo. Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imesema kutokana na ukuaji wa teknolojia nchini, inalenga kupeleka huduma za maktaba za kidijitali katika jamii, hasa katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, ili kuendana na mahitaji ya wasomaji wa sasa.
Hatua hiyo imekuja baada ya TLSB kufanya mabadiliko ya kidijitali ambayo yatafanya huduma hizo kuwafikia Watanzania wengi zaidi, kuvutiwa na kujenga tabia ya usomaji vitabu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Januari 19, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Dk Mboni Ruzegea, amesema Wilaya ya Rombo ni miongoni mwa wilaya zenye shule nyingi pamoja na vyuo, hivyo ni muhimu huduma hiyo kuwepo.
“Tunazindua maktaba ya Taifa ya kidigitali ambayo wananchi wataweza kusoma kupitia simu na kompyuta zao. Hii itakuwa ni huduma endelevu na itafikiwa na watu wengi,” amesema Dk Ruzegea.
Pia ameongeza, “Tuna mpango wa kitaifa wa kupeleka huduma za maktaba katika jamii, na kwa sasa tunaanza na maktaba ya shule ya Bustani iliyopo hapa Rombo, ambayo tayari imekamilika.”
Dk Ruzegea amesema kuanzishwa kwa maktaba hizo za kidijitali kutachochea jamii, hasa ikizingatiwa kuwa idadi ya wasomaji imepungua na watu wengi wanatumia mitandao zaidi kuliko vitabu.
“Tunaona umuhimu wa kuleta huduma hii hapa Rombo kutokana na wingi wa shule na vyuo. Huduma hii itachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha hamasa ya usomaji, hasa wakati huu ambao watu wengi wanapendelea kutumia mitandao,” amesisitiza Dk Ruzegea.
Nao baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wameelezea furaha yao kuhusu uwepo wa maktaba hizo za kidijitali.
Jesca Kalisti, mmoja wa wakazi wa Wilaya hiyo amesema kuwa huduma hiyo ni muhimu sana hasa katika nyakati hizi za sayansi na teknolojia. “Itasaidia sana kwa wananchi kupata taarifa muhimu kwa haraka na kwa urahisi kupitia vitabu, makala na tafiti,” amesema Jesca.
Aman Tesha, Mwananchi mwingine wa wilaya hiyo, amesema kuwa uwepo wa maktaba hizo utatoa fursa kwa wananchi kujifunza na kujiendeleza kimaarifa.
“Itachochea utamaduni wa kujifunza kila wakati na kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu kupata habari bila vikwazo,” amesema Tesha.
Pia amesema, maktaba za kidijitali zitatoa fursa kwa jamii ya wana Rombo kupata habari mpya zinazohusiana na maendeleo ya kisayansi, teknolojia, na masuala ya kijamii kwa haraka na kwa urahisi.