Dar es Salaam. Wakati leo Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, akiapishwa kuwa Rais wa 47 wa taifa hilo kubwa duniani, orodha ya viongozi waalikwa kwenye uapisho huo imewatenga viongozi wa Afrika.
Trump, aliyewahi kuwa Rais wa 45 kwenye uongozi wake wa 2017 hadi 2021, hakuwa na uhusiano mzuri na viongozi wa Afrika hadi anaondoka madarakani kwa kushindwa kwenye uchaguzi na Joe Biden.
Wakati wa mkutano wa 72 wa viongozi katika Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka 2017, Rais Trump ndipo alikutana kwa chakula cha mchana na viongozi wa Afrika waliokuwapo Umoja wa Mataifa, na baadaye alikutana na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Licha ya viongozi kadhaa wa Afrika kupongeza ushindi wa Trump dhidi ya mgombea wa Democrat, Kamala Harris, katika uchaguzi wa Rais wa Novemba mwaka jana, bado hakuna aliyepata mwaliko kulingana na orodha ya waalikwa iliyowekwa hadharani.
Kwa mfano, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Serikali yake imetoa taarifa kwamba kiongozi wao hakualikwa kwenye uapisho huo wa leo, licha ya Afrika Kusini kuwa washirika wa karibu wa Marekani.
Msemaji wa Ikulu, Vincent Magwenya, alithibitisha kwamba Rais Ramaphosa hajaalikwa kwenye uapisho huo.
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa, Clayson Monyela, alisema balozi wao nchini Marekani, Ebrahim Rasool, ataiwakilisha nchi.
Washirika wa Trump walioalikwa kwenye uapisho huo ni Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, Rais wa Argentina, Javier Milei, Rais wa zamani wa Brazili, Jair Bolsonaro, na Rais wa China, Xi Jinping.
Trump alipokuwa Rais kuanzia mwaka 2017–2021, hakuwahi kutembelea Afrika na alitoa kauli tata kuhusu nchi za Afrika kama vile Afrika Kusini, Ghana, Botswana, na Nigeria.
Pia, Trump aliwahi kutumia maneno ya dhihaka dhidi ya nchi za Afrika na Haiti, kauli iliyoshutumiwa na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Afrika huku wakimtaka aombe radhi, jambo ambalo hakuwahi kulifanya.
Wakati wa uongozi wake, uwekezaji wa Marekani katika nchi za Afrika ulipungua kutoka Dola bilioni 56.6 za Marekani hadi bilioni 46.9, ikiwa imepungua Dola bilioni 10.
Marais Afrika walivyompongeza Trump
Katika ukurasa wake wa X, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alimpongeza Trump kwa ushindi wa kihistoria, akieleza shauku yake ya kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ili kukuza amani, usalama, na maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, alituma salamu za pongezi kwa Trump kwa ushindi wake mkubwa, akisisitiza dhamira ya DRC kuendelea kushirikiana na kiongozi huyo mpya wa Marekani katika kukuza uhusiano wa kidiplomasia.
Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, alimpongeza Trump, akielezea ushindi huo kama wa kihistoria na kumtakia heri katika uongozi wake. “Nakutakia kila la heri unapoanza kuiongoza Marekani kwa mafanikio. Natumai tutaendelea kukuza ushirikiano wa nchi zetu,” alisema Rais Ndayishimiye.
Rais William Ruto wa Kenya naye alitoa pongezi kwa Trump kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani.
Vilevile, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, alimpongeza Trump kwa ushindi huo wa kihistoria, akisema, “Salamu za heri kwa ndugu zetu wa Marekani kufuatia ushindi wa Trump. Mafanikio haya yanaonyesha uhuru wa watu kuchagua viongozi wao. Tunatarajia kuendelea kukuza uhusiano wa nchi zetu.”
Rais wa Baraza la Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, pia alimtakia kila la heri Rais mpya wa Marekani, akitilia mkazo ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Mbali na viongozi wa Afrika, pia marais kama Vladimir Putin wa Urusi na Kim Jong Un wa Korea Kaskazini hawamo kwenye orodha ya viongozi waalikwa.
Trump wakati wa uongozi wake alifanya mkutano mara mbili na Kim Jong Un wa kutafuta suluhu ya silaha za maangamizi.
Mkutano wa kwanza ulifanyika Singapore mwaka 2018 na mkutano wa pili ulifanyika mwaka 2019 huko Hanoi, Vietnam.
Wengine ambao hawatahudhuria uapisho huo ni Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, pia Spika wa zamani wa Bunge, Nancy Pelosi, na Michelle Obama ambaye ni mke wa Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama.
Baridi yafanya Trump aapishwe ndani
Tofauti na ilivyozoeleka, hafla ya kuapishwa Trump itafanyika ndani ya jengo la Bunge la Capitol, kutokana na hali ya baridi kali katika jiji la Washington DC.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 40 kwa Rais mteule kuapishwa ndani ya jengo badala ya kwenye eneo la wazi.
Rais wa mwisho kuapishwa ndani ya jengo alikuwa Ronald Reagan mwaka 1985, alipokuwa akiapa kuanza muhula wake wa pili.
Pia, Trump wakati wa kuapa atatumia Biblia aliyopewa na mama yake mzazi sambamba na ile aliyotumia Abraham Lincoln.
Mwaka 1955 Trump alipewa Biblia hiyo na mama yake mzazi kwa ajili ya mafundisho kanisani huko New York.
Biblia ya Lincoln mara ya kwanza ilitumika Machi 4, 1861 kumuapisha Rais wa 16. Baada ya hapo ilitumiwa mara tatu; Barack Obama aliitumia mara mbili, muhula wa kwanza na muhula wa pili, na mara ya tatu ilitumiwa na Trump alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2017.
Trump ambaye alinusurika kuuawa wakati wa kampeni, uapisho wake unatarajiwa kuwa na ulinzi mkali zaidi ya ule wa mwaka 2017, ambapo mmoja wa walinzi wake alikuwa na mikono ya bandia huku akiwa amevaa koti kubwa na refu, ikiaminika mikono halisi ilikuwa imeshika silaha kali.
Pia, Trump amemteua mmoja wa walinzi wake waliomuokoa kwenye jaribio la mauaji kuwa mkurugenzi wa idara ya usalama.
Siku ya Martin Luther King
Uapisho wa Trump umeangukia siku ya Martin Luther King, ambayo ni sikukuu ya kitaifa nchini Marekani inayoadhimisha maisha na kazi ya kiongozi huyo wa haki za kiraia.
Siku hii hufanyika Jumatatu ya tatu ya Januari. Mwaka 1983, Rais Ronald Reagan alitia saini sheria ya kutoa mapumziko kwa siku hii kwa ofisi zote za Serikali, shule, na Wamarekani wote.
Hata hivyo, siyo mara ya kwanza kwa uapisho wa Rais kugongana na siku hii. Bill Clinton mwaka 1997 aliapishwa katika siku hii na Obama mwaka 2013 aliapishwa siku hii.