Prague: Imeelezwa kuwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Czech na Tanzania unazidi kuimarika kutokana na misingi imara ya ushirikiano wa kimataifa katika nyanja zote kwa sasa.
Kauli hiyo imetolewa jana Jumamosi Januari 18, 2025 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alipokutana na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Czech, Jan Lipavský na badaye kufanya mazungumzo na waandishi wa habari jijini Prague.
Waziri Kombo amesema Tanzania na Czech zina historia nzuri ya kidiplomasia iliyojengwa na waasisi wa mataifa hayo tangu miaka ya 1960. Hivyo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano huo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi.
Akiwa nchini Czech kwa ziara ya kikazi ya siku tatu aliyoianza Januari 16, 2025, Waziri Kombo amesema ziara hiyo ni ya kwanza mwaka huu na inalenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kimkakati yakiwamo ya uwekezaji, biashara, utalii, miundombinu, afya na elimu.
Kombo amesema jukumu la msingi kwa serikali zote ni kuhakikisha mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na wawekezaji.
“Lengo kuu la ziara yangu ni kuvutia kampuni za Czech kuwekeza Tanzania na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yanayokwamisha kasi ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi,” amesema Waziri Kombo.
Wakizungumzia uimarishaji wa sekta ya utalii, mawaziri hao walikubaliana kuharakisha kusainiwa kwa mkataba wa anga, ambao utawezesha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Czech.
Akizungumzia hilo, Waziri Kombo amesema idadi ya watalii kutoka Czech kuja Tanzania inaongezeka kila mwaka, huku Zanzibar ikipokea uwekezaji mkubwa kutoka kwa wawekezaji wa Czech katika sekta ya utalii.
Ametolea mfano uwekezaji wa kampuni ya Airplanes Africa Limited, ambayo imeanzisha kiwanda cha kutengeneza ndege aina ya Skyleader-600 mkoani Morogoro.
Amesema ndege hizo zina uwezo wa kutua katika mazingira magumu, jambo ambalo litaisaidia sekta ya utalii Tanzania.
Aidha, ameiomba Czech kushirikiana na Tanzania katika ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa (SGR), akibainisha kuwa Czech ina uzoefu mkubwa katika sekta hiyo.
Waziri huyo amehimiza ushirikiano wa moja kwa moja badala ya kupitia kampuni za kati.
Kwa upande wake, Waziri Jan Lipavský ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya Czech na Tanzania, hasa katika sekta ya anga na reli.
Ziara ya Waziri Kombo ni sehemu ya jitihada za utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi na alitembelea kampuni mbalimbali na kufanya mazungumzo na wawekezaji wakubwa walioonyesha nia ya kuwekeza Tanzania.