Wadau wa Kodi ambao ni wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Walipa Kodi Mkoani Kagera, wamekutana na Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi na kuwasilisha maoni, Kero changamoto na mapendekezo yenye lengo la kuboresha mfumo wa Ukusanyaji na Ulipaji Kodi hapa Nchini.
Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Balozi Ombeni Sefue imetawanyika maeneo tofauti kwa lengo hilo hilo la kukusanya Maoni hayo, kufuatia kilio cha walipa Kodi ambao mara kwa Mara wamekuwa wakipaza sauti zao kuhusiana na kile ambacho wanadai mfumo wa ulipaji kodi umekuwa sio rafiki, na zaidi ni kile kinachotajwa kuwa ni utitiri wa Kodi na tozo mbalimbali.
Kwa Mkoa wa Kagera, Sehemu ya Wajumbe wa Tume ya Rais ikiongozwa na Balozi Mwanaidi Maajar imepata nafasi ya kusikiliza na Kukusanya Kero, changamoto, maoni na mapendekezo kutoka kwa Wadau hao waliojitokeza katika Ukumbi wa Bukoba Sekondari, wakiwakilisha makundi mengine ya wafanyabiashara, na watoa huduma mbalimbali.
Miongoni mwa yale yaliyowasilishwa mbele ya Tume hiyo ni pamoja na, Uwepo wa Utitiri wa Kodi kwa Wafanyabiashara wanaoingiza au kuagiza Mizigo kutoka Nje ya Nchi (Exportation), Uwepo wa Tozo ya zuio kwa maeneo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa ni huduma (Withdraw Tax), Uwepo wa Mageti mengi ya Ulipaji Barabarani, lakini sambamba na kutotiliwa maanani agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya kufutwa kwa Madeni ya Nyuma ya Kodi ambazo hazikukusanywa Miaka ya Nyuma ya awamu iliyopita.
Akizungumza na Wanahabari mara baada ya Kikao hicho, Kiongozi wa Msafara wa Wajumbe wa Tume hiyo Balozi Mwanaidi Maajar amesema wao kama sehemu ya Tume ya Rais, wamepewa jukumu la kutathimini mfumo wote wa ulipaji Kodi, na ukusanyaji mapato na Tozo zote na kuwasilisha mrejesho na kushauri huo ili mfumo uweze kuleta Tija kwa pande zote mbili yaani Serikali na Wadau, na kuongeza kuwa Mkoa wa Kagera wamepata mawazo mengi mazuri ambayo yanagusa Mkoa wenyewe na mengine yakiwakilisha changamoto za Mikoa mingine.