Dar es Salaam. Wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Chadema, wanafanyiwa usaili leo Jumapili, Januari 19, 2025, ikiwa ni maandalizi ya kinyang’anyiro cha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika keshokutwa Jumanne Januari 21, 2025.
Usaili wa wagombea hao, unafanyika yalipo Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam na tayari wagombea mbalimbali wameanza kuwasili.
Wagombea wanaofanyiwa usaili huo ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar na Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Wanaogombea nafasi ya uenyekiti ni Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo, Tundu Lissu na Charles Odero.
Hadi saa 4:30 asubuhi, Odero ndiye mgombea uenyekiti pekee aliyekuwa amefika katika ofisi hizo, akisubiri taratibu za usaili, huku Lissu na Mbowe bado hawakuwa wamefika.
Kwa upande wa wanaogombea umakamu uenyekiti bara, John Heche na Ezekiel Wenje, nao hawakuwa wamefika ofisini hapo.
Wagombea wengine waliokuwa wamefika ofisini hapo ni wa ujumbe wa kamati kuu, baadhi waliketi katika eneo maalumu nje ya ofisi hizo, lililotengwa kwa ajili ya wasailiwa.
Mbali na wagombea, viongozi wa nafasi mbalimbali za Kanda, akiwemo Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ni miongoni mwa waliokuwepo katika ofisi hizo.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi….