Pemba. Watu wenye ulemavu kisiwani hapa wameiomba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuyapa kipaumbele makundi ya watu wenye mahitaji maalumu, katika uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
Awamu ya pili ya uandikishaji inatarajiwa kuanza Februari Mosi katika Wilaya ya Micheweni na kumalizika Machi 17 Wilaya ya Mjini Unguja huku tume ikitarajiwa kuandikisha wapiga kura wapya 78, 922.
Wananchi hao wametoa ombi hilo Januari 19, 2025 wakati wakizungumza na viongozi wa ZEC katika Halmashauri Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Maryam Kkhamis amesema kuna haja kwa tume kuyasimamia makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ili kuona wanapata kujiandikisha kwa wepesi kwenye daftari hilo, ili kupata haki yao ya kikatiba kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
“Hapa mara nyingi hasa watu wenye ulemavu wa akili, wamekuwa wakikosa kuandikishwa kwa watu kutotambua mgonjwa wa akili na mlemavu wa akili. Hapa tunaomba suala hili tume iliangalie kwa karibu tusije kukosa kuandikishwa tukakosa haki yetu ya kikatiba kushiriki katika uchaguzi mkuu,” amesema.
Mwingine Awena Khamis Rashid amesema mbali ya changamoto hiyo pia muda uliowekwa ni mchache, hivyo ipo hatari ya wengine kukosa fursa hiyo ikizingatiwa ni awamu ya mwisho ya kujiandikisha.
“Wengine wanaweza kuwa mbali kutokana na harakati za kiuchumi, tunaomba ZEC iongeze muda wa uandikishaji maana muda wa siku tatu tunaona bado ni kidogo,” amesema.
Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina alisema changamoto walizozieleza wananchi hao, watazifanyia kazi kwa karibu kuona kila mmoja anapata nafasi ya kujiandikisha ili kupata haki yake ya msingi ya kupiga kura.
Amesema wameyaita makundi hayo kusikiliza changamoto na ushauri wao kwani na wao ni sehemu ya wanajamii wana haki ya kushiriki kama wananchi wengine kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.
Kuhusu tatizo la muda, amesema wataangalia kwa kiasi gani idadi ya wananchi watakaojitokeza kujiandikisha watahakikisha kila mwenye vigezo kwa mujibu wa sheria anaandikishwa.
“Lengo la kuita haya makundi ni kutoa changamoto zao na kushauri, tumesikia na tutakwenda kuzifanyia kazi kabla ya kazi yenyewe kuanza na kumalizika,” amesema Faina
Naye Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Aziza Iddi Suwed amesema awamu ya pili ya uandikishaji itahusisha wote wenye sifa waliotimiza umri wa miaka 18 na ambao walishindwa kujiandikisha awamu iliyopita.
“Tunawaomba wananchi wenye sifa wajitokeze kujiandikisha daftari litakapoanza na wale watakaohakiki taarifa zao au uhamisho watumie muda huo waweze kuweka mambo sawa wapate haki yao ya msingi ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao,” amesema.
Pia, Jaji Aziza amewasihi wananchi hao kufuatilia vitambulisho vyao mapema vitakavyowasaidia kupata wepesi wa kujiandikisha katika daftari hilo pindi litakapoanza.