Dar es Salaam. Wenyeviti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka mikoa 21, wametoa tamko rasmi la kumuunga mkono Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Taifa.
Viongozi hao wanatoka katika mikoa ya Mara, Ruvuma, Katavi, Simiyu, Rukwa, Songwe, Ubungo, Mtwara, Ilala, Kaskazini Unguja, Geita, Kagera, Singida, Tabora, Lindi, Kigoma, Njombe, Mjini Magharibi na Kusini Unguja.
Wakizungumza leo Jumapili Januari 19, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wenzao, viongozi hao wamesema Lissu anavutia wananchi kutokana na mvuto wake na sera zake zinazolenga mabadiliko ya kweli ndani ya chama na taifa kwa ujumla.
Wakili Alfred Sotoka, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Rukwa aliyesoma tamko hilo, amesema Lissu anakubalika ndani na nje ya chama na kwamba, anaweza kuleta mabadiliko wanayohitaji.
Viongozi hao wametoa tamko hilo zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kufanyika kwa shughuli ya kupiga kura, ambapo Tundu Lissu anakabiliana na upinzani mkubwa kutoka kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, pamoja na kada wa chama, Charles Odero.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya viongozi hao 21, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Rukwa, Sotoka, amesema sababu zilizowafanya kumuunga mkono Lissu.
“Tunatangaza rasmi kwa umoja wetu kuwa tunamuunga mkono Lissu, tukiwa na wapiga kura nyuma yetu. Tunamuunga mkono kwa sababu ana mvuto mkubwa kwa wananchi, anakubalika kwa sasa ndani na nje ya chama, na ana uwezo wa kuleta mabadiliko tunayoyahitaji,” amesema Sotoka.
Amesema miongoni mwa mambo yanayowashawishi kumuunga mkono Lissu ni sera zake, ikiwemo ile ya kushusha fedha hadi ngazi ya majimbo.
Amebainisha kuwa, kwa sasa fedha hazishuki licha ya kwamba mwaka 2015 walipata idadi kubwa ya wabunge.
“Ilikuwa tukipiga kelele tunajibiwa makamanda pigeni kazi, fedha ni kwa ajili ya uchaguzi wa 2020. Hata hivyo, jambo lingine ni kwamba tunakosa hata fedha za kulipia ofisi kwa wale tuliopanga,” amedai kiongozi huyo.
Aidha, Sotoka amesema sera nyingine ya Lissu inayowavutia ni ukomo wa madaraka, hasa kwenye nafasi za ubunge wa viti maalum, anapendekeza kuwepo utaratibu wa kutoa nafasi kwa wengine pia.
“Tunahitaji uendeshaji wa chama kwa uwazi. Hata tukipata fedha kidogo, tujue namna zinavyotumika. Lissu amekuja na sera hizi na sisi kama viongozi tumevutiwa nazo na tunaona italeta unafuu,” amesema.
Amesema Lissu anaonyesha ujasiri wa kupambana na vitendo vya rushwa ndani na nje ya chama, hatua muhimu kwa ustawi wa chama na wananchi wanaokumbana na changamoto mbalimbali.
“Chama hiki, ili kiweze kupata nguvu mpya, ni lazima tumchague mtu ambaye umma, wanachama, na wapenzi wanamtaka kuwa kiongozi. Huyo ni Lissu. Hatupaswi kudharau maoni ya wananchi. Kuna wanaosema wanaozungumza si wapiga kura, lakini sisi tuko hapa kwa niaba yao. Baada ya kumaliza uchaguzi wa ndani, tunaenda kwenye uchaguzi wa nje. Tukiwadharau sasa, tutawaambia nini?” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa ni muhimu kusikiliza maoni ya wananchi kwa sababu baada ya uchaguzi wa ndani, kazi kubwa itakuwa ni kutafuta wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais.
“Tunahitaji uongozi wa uwazi ili tuweze kusonga mbele,” amesema muwakilishi huyo.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Songwe, Isakwisa Thobias amesema mkoani kwake kuna jumla ya kura 25, kati ya hizo, kura 20 zinaelekea kumuunga mkono Lissu, huku kura tano zilizobakia zikigawanyika; tatu zikienda kwa Mbowe na mbili zikiwa bado hazijafikiwa uamuzi.
“Bado nafanya mazungumzo na wamiliki wa kura hizo mbili ambazo hazijaeleweka. Ni lazima tufanye mabadiliko kwa sababu wananchi wanayahitaji, na Wanasongwe wanamtaka Lissu,” amesema Isakwisa.
Kwa upande wake, Kada wa Chadema na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, amewahimiza viongozi hao kusimamia kile wanachoamini kuwa sahihi, ikiwa wanataka kuona mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya chama na wananchi.