Faida, hasara minyukano ya vigogo Chadema

Dar es Salaam. Minyukano ya viongozi na wanachama wa Chadema wanaomuunga mkono Mwenyekiti wao Freeman Mbowe na wanaomuunga mkono Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, imetafsiriwa kwa sura mbili tofauti.

Sura ya kwanza imetajwa kuwa mbaya inayolenga kukibomoa chama hicho, huku wengine wakiamini kuwa minyukano hiyo inathibitisha uwazi na kuwakumbusha viongozi kwamba hakuna siri katika uendeshaji wa vyama.

Uchaguzi mkuu wa chama hicho, utafanyika kesho Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam.

Tangu Lissu alipoweka wazi azma yake ya kugombea uenyekiti wa chama hicho, kumekuwa na mivutano kati ya wanaomuunga mkono na wale wanaomuunga mkono Mbowe.

“Kama minyukano hii itaendelea baada ya uchaguzi wao, hakuna shaka kwamba itakuwa na athari kubwa kwenye chama hadi kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba,” amesema Dk Sabatho Nyamsenda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nyamsenda anaitazama minyukano hiyo kama afya ndani ya chama endapo itakoma mara tu baada ya uchaguzi wao.

“Itakuwa na athari kwa namna Chadema itakavyojipanga baada ya uchaguzi huo, ikiendelea si ajabu kuwepo na mpasuko ndani ya chama.

“Sitaki kuwa mtabiri kuonyesha yupi atashinda, lakini kibarua cha kwanza kwa atakayekalia kiti hicho ni kuweka masilahi yake pembeni na kukijenga chama, kuondoa makundi na kufanya mabadiliko kwa kuwa minyukano inayoendelea inaonyesha kiini cha tatizo,” amesema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe anasema minyukano hiyo ni sahihi japo inafanyika wakati ambao si sahihi.

“Chama makini kinapaswa kwenda kwenye uchaguzi mkuu kikiwa kimetulia, siamini kama kufikia Septemba au Oktoba makovu wanayoyaweka sasa yatakuwa yamepona ili kuingia kwenye uchaguzi mkuu,” amesema.

Amesema mara nyingi uchaguzi wa ndani wa chama huwa anaacha makovu, na ndivyo itakavyokuwa kwa Chadema.

“Wakati huu si rafiki kwao kufanya haya kwani ni vigumu kuanzia Januari 22 hadi Oktoba wawe wametibu majeraha,” anasema.

Amesema, mgombea atakayeshinda nafasi ya mwenyekiti atakuwa na kibarua cha kutibu majeraha na kukirudishia chama amani kwa kuishawishi kambi iliyoshindwa kurudi mezani.

“Kama watakwenda kwenye uchaguzi mkuu bila kuwa wamoja, itakuwa ni turufu ya kushindwa,” amesema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amekuwa tofauti akieleza minyukano hiyo haina afya kwenye chama hicho kwani huo ni uchaguzi wao wa ndani ambao haukupaswa kuwavuruga wenyewe kwa wenyewe.

“Kinachofanyika Chadema sasa hakuna shaka kitakuja kutumiwa na wapinzani wao kuwabomoa kwenye uchaguzi mkuu ujao,” amesema Dk Mbunda.

Amesema, Mbowe ni kiongozi aliyewahi kusisitiza kuamini kwenye maridhiano yanayoleta faida.

“Ile hali anayoiamini kwenye maridhiano ianzie ndani, ukiangalia Chadema hivi sasa kimegawanyika kuna kambi mbili, japo wapo wanaodhani kinachofanyika kinaonyesha demokrasia, lakini walikofika sasa ni kubaya.

“Mwanzoni wengi walidhani wanachokifanya Chadema ni kutaka kukihuisha chama kwa kuwa kilikuwa kimepoa, lakini ingekuwa ni hivyo ingekuwa ni kwa kiasi ni wakakubaliana kitu gani kitolewe na kipi kisitolewe kwa wananchi, lakini wanapokwenda si hivyo,” amesema Dk Mbunda.

Amesema namna pekee ya kurekebisha hayo yanayoendelea sasa ni kutumia wiki hii ya mwisho kuendesha vikao vya maridhiano ya ndani ambavyo vitaamua suluhu ya kuwafanya kuwa wamoja na si kubomoana wenyewe kwa wenyewe.

“Kama hali itaendelea hadi kwenye uchaguzi wao, Mbowe akishinda ni wazi atawakosa watu muhimu katika chama chake na akishinda Lissu naye hatapata watu wa kuwaongoza vizuri kama hakutakuwa na maridhiano,” amesema.

Hata hivyo, mchambuzi wa siasa, Dk Paul Loisulie amesema minyukano ya viongozi anaiona kwa mtazamo chanya kwa kuwa inadhihirisha chama hicho kimejenga utaratibu wa kuwa wazi kwenye ushindani wa demokrasia.

“Hii itawaletea manufaa siku zijazo, kwani hivi sasa kiongozi yoyote wa Chadema atajua hakuna siri duniani.

“Japo shida itakuwa pale ambapo minyukano hii itaendelea hata baada ya uchaguzi wao, itakuwa na athari na huenda ikasababisha anguko la Chadema.

Hata hivyo, mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Chadema, Profesa Azaveli Lwaitama amesema kinachofanyika kwa viongozi wao kinaonyesha ni ukomavu wa demokrasia.

“Wala si tatizo, kwa kuwa tunaionyesha dunia kwamba mnaweza kunyukana vikali kwenye harakati za uchaguzi, kisha ukiisha mnakuwa wamoja na ndicho kitakachotokea,” amesema alipozungumza na Mwananchi.

Ameongeza, “Binafsi sioni kama kuna tatizo hata baada ya uchaguzi kupita, akishinda Mbowe, sidhani kama atamuacha Lissu na akishinda Lissu, Mbowe ataendelea kuwa Chadema kama mjumbe wa kudumu kwa mujibu wa katiba yetu.

“Ninavyojua mimi, Mbowe na Lissu hawana ugomvi, ninawaona kwenye mikutano, shida ni wapambe, huwa nasema atakayeshinda hatakiwi kuendelea kuwasikiliza hao wapambe, kwani wote wawili wanategemeana.”

Miongoni mwa wanaomuunga mkono Lissu ni mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho John Heche, ambaye Januari 5, 2025 alitangaza kuwania umakamu mwenyekiti wa chama hicho, huku upande wa Mbowe ukiungwa mkono na Ezekia Wenje aliyetangaza kuwania nafasi hiyo pia.

Upande wa Lissu pia unaungwa mkono na aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, ambaye Januari 14, 2025 alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akieleza kiini cha mgogoro.

Maelezo ya Lema yalimwibua Wenje ambaye naye alijibu mapigo akidai kuwapo kwa njama za kumpindua Mbowe zilizopangwa kutekelezwa na kundi la Lissu kwa kutumia michango ya fedha za ‘Join the Chain’.

Kama hiyo haitoshi, Lema naye kesho yake akaitisha mkutano wa waandishi wa habari, akihusisha makada wengine walio upande wa Lissu kujibu tuhuma zilizoibuliwa na Wenje.

Mbowe mwenyewe akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita, aliwakosoa vikali Lema, Heche na Lissu, akiwataja kuwa viongozi walioleta kiburi, jambo ambalo hakukubaliana nalo.

Mbali na majibizano hayo, kumekuwa na matamko kutoka kwa viongozi wa mikoa, kanda na majimbo wakieleza kumuunga mkono Lissu.

Kanda zilizotoa matamko ya kumuunga mkono Lissu Serengeti na Victoria, huku pia baadhi ya wenyeviti wa mikoa wakitoa matamko hayo, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela aliyezungumza na waandishi wa habari.

Januari 19, 2025 wenyeviti 21 wa Chadema walitangaza pia kumuunga mkono Lissu jijini Dar es Salaam, lakini siku hiyohiyo, baadhi ya viongozi wakiwamo wenyeviti watatu wa mikoa walijitokeza wakisema wanamuunga mkono Mbowe.

Mvutano pia ulionekana kwenye chaguzi za mabaraza, ambapo mchuano mkali ulikuwa Baraza la Vijana (Bavicha), ambapo Deogratius Mahinyila anayemuunga mkono Lissu alishinda.

Katika Baraza la Wazee (Bazecha), aliyeshinda ni Susan Lyimo, ambaye licha ya kutokuweka wazi anatajwa kuwa upande wa Mbowe, huku Baraza la Wanawake (Bawacha), aliyeshinda ni Sharifa Suleiman na ametangaza kumuunga mkono Mbowe.

Related Posts