Israel yawaachia huru Wapalestina 90 kutoka magerezani

Gaza. Wafungwa 90 raia wa Palestina wameachiwa kutoka katika magereza ya Israel.

Wafungwa hao ni wanawake na watoto waliokamatwa na Jeshi la Israel (IDF) na kufungwa katika magereza nchini humo.

Wafungwa hao wameachiwa usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 20, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kusitishwa kwa vita kati ya Jeshi la Israel na Kundi la Hamas la Gaza nchini Palestina.

Kuachiwa kwa wafungwa hao ni matokeo ya Hamas kuwaachia wateka watatu wa Israel waliokuwa wakishikiliwa eneo la Gaza na wapiganaji hao tangu Oktoba 7, 2023, ambao ni Romi Gonen (24) , Emily Damari (28) na Doron Steinbrecher (31) waliokabidhiwa kwa maofisa wa kikosi cha Msalaba Mwekundu.

Israel baada ya kuwaona raia wake nayo imewaachia wafungwa 90 ambao ni wanawake na watoto.

Tayari wafungwa hao wamewasili eneo la Gaza na kupokelewa na maelfu ya wapendwa wao.

Miongoni mwa walioachiwa na mwanasiasa mashuhuri wa Chama cha Popular Front for Liberation of Palestine (PFLP) Khalida Jarrar, ambaye alikamatwa kutokana na harakati zake za kupinga kupingana na utawala wa Kizayuni eneo la Gaza.

Jarrar, alifungwa na mamlaka za Israel kutokana na kauli zake ambazo Israel ilidai ni za kichochezi zilizotokana na hotuba zake kwa umma.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Al Jazeera, Nida Ibrahim, miongoni mwa walioachiwa ni watoto ambao walikamatwa na IDF kwa makosa ya kuwarushia wanajeshi mawe walipokuwa wakifanya uvamizi eneo la Gaza.

“Mamia ya majina ya raia wa Palestina yametangazwa kuwa wataachiwa kutoka kwenye magereza ya Israel na wote wanatumikia vifungo vilivyoratibiwa na utawala wa Israel.  Vifungo hivyo ni mbinu iliyokuwa ikitumiwa na Israel kuwatisha raia wa Palestina.

“Vifungo hivi vimekuwa vikiendelea kurejeshwa kwa raia kila mara wanapokamatwa na wanajeshi wa Israel,” amesema.

Kwa mujibu wa kamisheni ya wafungwa na wafungwa walioachiwa ya Palestina, kuna Wapalestina zaidi ya 10,000 wanaoshikiliwa kama wafungwa eneo la West Bank katika magereza ya Israel.

Idadi kamili ya Wapalestina ambao wanashikiliwa na kuwekwa vizuizini nchini Israel tangu kuanza kwa mapigano hayo Oktoba 7, 2023, bado haijafahamika hadi sasa.

Mfungwa maarufu,  Jarrar, kabla ya kukamatwa kwake na IDF alikuwa mbunge katika Bunge la Palestina na taarifa za kukamatwa kwake nchini Israel ziliwashtua wengi ulimwenguni, huku akidaiwa kutengwa peke yake gerezani.

Vita ya Israel na Hamas imesababisha vifo vya raia 46,913 wa Palestina na kujeruhi 110,750 tangu Oktoba 7, 2023. Wakati huo, raia 1,139 waliuawa nchini Israel wakati wa uvamizi wa Hamas huku zaidi ya 200 wakichukuliwa mateka na wapiganaji hao.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts