Jela miaka 15 kwa kumuua mkewe bila kukusudia

Geita. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Geita imemhukumu kifungo cha miaka 15 jela, Andrea George (21) kwa kosa la kumuua mkewe, Tabu Jems bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo,  Kelvin Mhina baada ya kusikiliza kesi hiyo iliyokuja mahakamani hapo leo Januari 20,2025 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).

Mwendesha mashitaka wa Serikali, Wakili Scolastica Teffe akisoma maelezo ya awali ya mshtakiwa, ameieleza Mahakama kuwa Juni 13,2024 huko katika kijiji cha Nyakahengele B kata ya Ihanamilo wilayani Geita, mshtakiwa alimuua mkewe bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio marehemu Tabu Jems akiwa na mdogo wake Naomi wakitokea eneo la Nyakahengele A walikutana na mshtakiwa ambaye aliomba kuzungumza na mkewe (Tabu) kwa kuwa walikua wameachana, mkewe aligoma kwenda kuzungumza naye.

Amedai baada ya mkewe kukataa mshtakiwa alitoa panga alilokuwa ameficha kwenye nguo na kuanza kumshambulia nalo sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani, shingoni na kwenye mikono hali iliyosababisha kifo chake.

 “Mdogo wake alikimbia na kuomba msaada kwa majirani ambao walifika na kutoa taarifa polisi na polisi walipofika waliuchukua mwili na kumkamata mshtakiwa aliyekua amejificha kwenye nyumba ya jirani,” ameeleza Teffe.

Ameieleza Mahakama kuwa baada ya mshtakiwa kukamatwa aliwaonyesha polisi alikoficha panga lenye damu na mwili wa marehemu ulipofanyiwa uchunguzi daktari alieleza sababu za kifo ni kuvuja damu nyingi, iliyotokana na majeraha aliyoyapata hususani sehemu ya ubongo na mshipa mkubwa kwenye shingo.

Kutokana na maelezo hayo mshtakiwa alikiri kuua bila kukusudia na kutiwa hatiani chini ya kifungu cha 195 na 198 cha makosa ya jinai kilichorejelewa mwaka 2022.

Wakili Teffe ameieleza Mahakama hakuna kumbukumbu ya mshtakiwa huyo kutenda makosa mengine ya jinai, lakini akaiomba Mahakama kwa kosa hilo izingatie silaha iliyotumika kwenye tukio ikizingatiwa marehemu alipata majeraha makubwa kichwani, shingoni na kwenye viganja ambayo ni wazi yangeweza kusababisha kifo, na kuomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho.

Wakili wa utetezi, Jesca Materu aliomba mteja wake apunguziwe adhabu kwa kuwa amekiri kosa na hajaisumbua Mahakama hivyo ameonyesha kujutia kosa alilolitenda.

Amedai kuwa mshtakiwa ni kijana mdogo wa miaka 21 na bado anategemewa na familia hususan mtoto wake wa miaka miwili na tayari amekaa mahabusu kwa miezi minane, lakini pia ni kosa la kwanza kutendwa na mshtakiwa.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Mhina amesema kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani  mtu akikiri kosa Mahakama inapaswa imfikirie na kwa mujibu wa wakili wake kitendo cha mshtakiwa kukiri ni kuonyesha kujutia.

Amesema kifo hicho kingeweza kuepukika kwa kuwa walikua wameshaachana na kama marehemu alikua hataki kurudi, mshtakiwa alikua na uwezo wa kutumia njia nyingine za kumuomba arudi badala ya kuchukua panga na kuanza kumkata.

Ili kutenda haki Jaji Mhina amesema Mahakama hiyo inamfunga mshtakiwa miaka 15 jela kwa kosa la kuua bila kukusudia na endapo hajaridhika na hukumu iliyotolewa ana haki ya kukata rufaa.

Related Posts