Kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas wa Palestina, watu waliokuwa wakishikiliwa mateka kutoka pande zote mbili wameanza kuachiwa.
Video mbalimbali zinaendelea kusambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, zikionesha mateka watatu wa Israel wakiachiwa jana Jumapili.
Taarifa zinaeleza kuwa baada ya Hamas kuwaachilia mateka hao watatu, Israel nayo imewaachilia mateka 90 wa Palestina katika siku ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita.
Mamia ya wananchi wa pande zote mbili walionekana wakiwa na furaha kubwa kuwapokea wapendwa wao baada ya mapigano yaliyodumu kwa takribani miezi 15 na kusababisha maafa makubwa, hasa upande wa Palestina.