Ramovic ashtukia kitu Yanga, ajibebesha zigo la lawama

MASHABIKI wa Yanga usiwasogelee wala usiongee nao kwani bado hawaelewi kipi kilichoizuia timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa suluhu na MC Alger ya Algeria, lakini kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic ametuliza upepo huku akitaja dira na mwelekeo mpya.

Yanga ililazimishwa suluhu na MC Alger katika mechi ya mwisho ya Kundi A ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, iliyoifanya ifikishe pointi nane kama ilizovuka nazo msimu uliopita, lakini wapinzani wao wakinufaika kwa kufikisha alama tisa na kuungana na Al Hilal ya Sudan iliyoongoza msimamo wa kundi.

Kutokana na matokeo hayo tangu juzi usiku mashabiki na wapenzi wa Yanga wamewaka na kulalamika, lakini kocha wa timu hiyo, Ramovic amewatuliza kwa kuwaeleza kuwa soka ndivyo lilivyo, lakini bado wana nafasi ya kujipanga upya kutimiza malengo waliyonayo kwa msimu huu ili warudi tena kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ramovic aliyeiongoza Yanga katika mechi 11 tangu alipoteuliwa kumpokea, Miguel Gamondi aliyefurushwa baada ya kupoteza michezo miwili ya Ligi Kuu, mbele ya Azam FC na Tabora United, alisema hawana namna zaidi ya kukubali kuwa safari ya kimataifa imeishia hapo msimu huu na sasa wanarudi kuangalia mashindano ya ndani yanayorudi wikiendi hii.

Ramovic alisema wanakwenda kujipanga sawasawa kurudi kwa nguvu kwenye mashindano ya ndani ili kutetea mataji ya Ligi Kuu Bara na Azam Shirikisho, ili kusaka tiketi ya michuno ya kimataifa kwa msimu ujao, hivyo kutaka kila Mwanayanga kutulia na kuendelea kuiunga mkono timu hiyo.

Yanga itaanza kucheza kiporo cha michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Copco FC ya Mwanza wikiendi hii kabla ya kucheza kiporo kingine cha raundi ya 16 ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.

“Hatuna namna bali kukubaliana na ukweli kuwa tumeishia hapa katika Ligi ya Mabingwa, yapo ambayo tumejifunza kwa kutolewa kwetu, lakini sasa tutaelekeza akili yetu kwa nguvu zote kwenye mashindano ya Ligi na Kombe la Shirikisho (TFF), “alisema Ramovic na kuongeza;

“Nafahamu namna mashabiki wetu wameumizwa na haya matokeo hali hiyo pia imetukumba hata sisi makocha, wachezaji na hata viongozi wetu lakini tuna safari bado ya kwenda kusimamia malengo yetu msimu huu.”

Kocha huyo aliongeza kuwa anachoondoka nacho kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa ni kwamba wanatakiwa kuandaa timu yao kwa ujazo mkubwa wa kucheza soka la ushindani mkubwa tofauti na ushindani wanaoupata kwenye mechi za Ligi ya ndani.

“Ukiona haya mashindano ya Ligi ya Mabingwa utaona kuna namna tunatakiwa kuongeza ubora wetu zaidi, kwani kuna tofauti kubwa kati ya ushindani wa ligi ya ndani na mechi za Ligi ya Mabingwa,” alisema kocha huyo raia wa Ujerumani aliyeongeza;

“Tutakwenda kujipanga zaidi kutengeneza timu bora ya ushindani, hili ni eneo langu, najua namna nitapambana nalo ili msimu ujao turudi tukiwa na hali tofauti ya ubora wa kikosi chetu.”

Chini ya Ramovic katika Ligi ya Mabingwa, Yanga imevuna pointi nane kupitia mechi sita za makundi ikifunga mabao matano na yenyewe kufungwa sita, wakati katika Ligi Kuu imecheza mechi tano na kuvuna pointi 15, kwani imeshinda zote na kufunga jumla ya mabao 10 na yenyewe kuruhusu mawili tu.

Yanga ilianza mechi za makundi kwa kupoteza 2-0 mara mbili mfululizo mbele ya Al Hilal na MC Alger, kisha kutoka sare ya 1-1 na TP Mazembe ya DR Congo iliyokuja kuifumua Kwa Mkapa kwa mabao 3-1 kisha kwenda kuichapa Al Hilal ikiwa kwao na kumalizia na suluhu na MC Alger.

Katika Ligi chini ya Ramovic, Yanga ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 ugenini mbele ya Namungo, kisha kuichapa Mashujaa kwa mabao 3-2 na baadaye 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons zote ikiwa nyumbani na kuifuata Dodoma Jiji na kuishindilia pia 4-0 na kumalizana na Fountain Gate iliyoinyuka 5-0.

Related Posts